Habari Mseto

Gavana Nyoro ahimiza haja ya hamasisho kuhusu BBI

November 17th, 2020 1 min read

Na SAMMY WAWERU

GAVANA wa Kiambu James Nyoro ameeleza umuhimu wa kufanya hamasisho la ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI) kwa umma ili Wakenya waelewe yaliyomo.

Bw Nyoro amesema ‘masomo’ ya ripoti hiyo kwa umma, ni hatua muhimu kabla kufanya uamuzi wowote.

“Hamasisho la yaliyomo kwenye BBI ni muhimu kabla kufanya uamuzi wowote, na ndio maana ninaendelea kukutana na watu kuwaelimisha na kupokea maoni yao,” akasema Gavana huyo.

Bw Nyoro amekuwa akiandaa mikutano mbalimbali na wakazi wa Kiambu na kuhamasisha kuhusu BBI, huku akikusanya maoni na mapendekezo yao.

Baadhi ya masuala anayosema wenyeji wa Kiambu wanasisitiza kutekelezwa na ripoti hiyo ni pamoja na usawa katika uongozi, usambazaji wa pesa mashinani kupitia ugatuzi, kina mama, vijana na walemavu kujumuishwa katika uongozi.

Baada ya salamu za maridhiano kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM, Raila Odinga mnamo Machi 2018, walibuni jopokazi la BBI, lililokusanya maoni ya wananchi, viongozi, mashirika na wadau mbalimbali nchini, katika kile viongozi hao walihoji ni oparesheni kuunganisha taifa.

Ripoti ya Mpango huo wa Maridhiano ilizinduliwa rasmi Oktoba 2020, na wabunge na viongozi wanaoiunga mkono chini ya vuguvugu la ‘Kieleweke’ waliafikiano kuipitisha bila kuifanyia marekebisho, licha ya kukosolewa na Naibu Rais William Ruto na kikosi chake cha ‘Tangatanga’.

Endapo ripoti hiyo itapitishwa na mabunge yote, kuanzia bunge la kitaifa, seneti na mabunge ya kaunti, kura ya maamuzi kubadilisha Katiba ya sasa na iliyozinduliwa 2010, itaandaliwa.