Gavana Ottichilo atimiza ahadi ya kuwapa Vihiga Queens Sh1 milioni

Gavana Ottichilo atimiza ahadi ya kuwapa Vihiga Queens Sh1 milioni

Na GEOFFREY ANENE

MABINGWA wa soka ya klabu za akina dada ya Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) Vihiga Queens wametunukiwa Sh1 milioni na Gavana wa Kaunti ya Vihiga, Wilber Ottichilo mnamo Septemba 25.

Gavana huyo alikuwa ameahidi timu hiyo kitita hicho baada ya kufuzu kuwa mwakilishi wa Cecafa kwenye makala ya kwanza ya Klabu Bingwa Afrika nchini Misri mwisho wa mwaka 2021.

“Jumamosi, tumeandaliwa dhifa ya chakula cha mchana na kaunti yetu ya Vihiga na Gavana Ottichilo aliyetumia fursa hiyo kutimiza ahidi yake ya kututuza Sh1 milioni. Asante sana Gavana kwa kutimiza ahadi na tutazidi kutia bidii,” Vihiga Queens ilitangaza.

Vihiga Queens walijikatia tiketi ya kushiriki kombe hilo baada ya kupepeta wanabenki wa CBE kutoka Ethiopia 2-1 kwenye fainali ya kusisimua ya Cecafa ugani Kasarani mnamo Septemba 9.

Mshambuliaji matata Jentrix Shikangwa alifungia Vihiga mabao yote mawili katika mechi hiyo iliyohudhuriwa na Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) Fatma Samoura.

Mabingwa hao wa zamani wa Kenya, ambao walitiwa makali na kocha mkuu wa timu ya taifa ya Kenya Charles Okere na kocha mkuu wa Vihiga Queens Boniface Nyamunyamu, walikuwa wamepoteza 4-2 dhidi ya Waethiopia katika mechi za Kundi B.

Shikangwa aliibuka mchezaji bora wa mashindano hayo yaliyovutia klabu nane kutoka mataifa ya Kenya, Ethiopia, Uganda, Tanzania, Burundi na Djibouti pamoja na Zanzibar.

Siku ya ushindi huo, Vihiga walizawadiwa Sh3,297,900 na Baraza la Mashirikisho ya Soka ya Afrika Mashariki na Kati (Cecafa). CBE waliridhika na Sh2,198,600 nao Lady Doves kutoka Uganda waliolima Simba Queens ya Tanzania 2-1 katika mechi ya kutafuta mshindi wa medali ya shaba, wakatia kibindoni Sh1,099,300.

Timu hiyo ya Kenya itawania taji la Klabu Bingwa Afrika dhidi ya wenyeji Wadi Degla SC (Misri), AS FAR kutoka Morocco (washindi wa Muungano wa Kaskazini mwa Afrika), AS Mande kutoka Mali (washindi shindano la kwanza la Muungano wa Magharibi mwa Afrika), Hasaacas Ladies kutoka Ghana (washindi shindano la pili la Muungano wa Magharibi mwa Afrika) na Rivers Angels (nambari mbili katika shindano la pili la Muungano wa Magharibi mwa Afrika).

Washindi kutoka Muungano wa Afrika ya Kati kati ya Malabo Kings (Equatorial Guinea) na FCF Amani (DR Congo) pamoja na Baraza la Mashirikisho ya Soka ya Kusini mwa Afrika (Cosafa) Mamelodi Sundowns Ladies pia watashiriki dimba hilo.

You can share this post!

Wanafunzi kadhaa Juja washindwa kujiunga na Kidato cha...

FUNGUKA: ‘Yote kwa raha zangu’