Habari MsetoSiasa

Gavana taabani kuhusu sakata ya mitungi ya kunawa mikono

April 12th, 2020 2 min read

VALENTINE OBARA na BRIAN OJAMAA

BUNGE la Kaunti ya Bungoma linataka asasi za serikali za kupambana na ufisadi zichunguze madai kwamba serikali ya kaunti hiyo inayoongozwa na Gavana Wycliffe Wangamati ilinunua mitungi midogo ya maji kwa Sh10,000 kila mmoja.

Taarifa kutoka kwa bunge hilo jana ilisisitiza kuwa kikao kitaitishwa kujadili madai ya sakata hiyo hapo Jumanne, Aprili 14.

“Spika alipokea na akakubali ombi la kamati kufanya vikao vya kuchunguza madai ya ubadhirifu wa fedha zilizonuiwa kusaidia kupambana na virusi vya corona. Vikao viliahirishwa ili kuwezesha mashauriano kuhusu jinsi vitakavyofanyika kwa njia inayozingatia maagizo ya serikali kuhusu kuzuia ueneaji wa corona,” ikasema taarifa hiyo.

Alhamisi iliyopita, Seneta wa Bungoma, Bw Moses Wetang’ula aliungana na madiwani wa kaunti hiyo kukashifu madai kwamba utawala wa Bw Wangamati ulinunua mitungi ya maji ya lita 20 kwa Sh10,000 kila mmoja.

Jana, Bw Wangamati alijitetea dhidi ya madai hayo akisema mitungi hiyo yote iliyosambazwa katika masoko mbalimbali ilikuwa imefadhiliwa na wahisani. Hata hivyo, alikataa kutaja wahisani wahusika.

“Kuna wanasiasa wanaotaka kutumia suala la Covid-19 kisiasa na kuleta uhasama. Hatujawahi kutumia pesa za kaunti hii kununua mtungi wa lita 20. Mitungi yote 368 iliyosambazwa ilikuwa ya lita 120 na yote ilifadhiliwa na wahisani,” akasema. Bw Wangamati alitaka mtu yeyote aliye na ushahidi kuwa fedha za umma zilitumiwa vibaya kwa ununuzi wa mitungi hiyo, awasilishe ushahidi kwa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC).

“Kama kuna yeyote aliye na ushahidi kwamba afisa yeyote katika serikali yangu alilipa Sh10,000 kununua mtungi mmoja, alete ushahidi huo au aupeleke kwa EACC, Bunge la Kaunti au asasi nyingine husika. Tuna janga la kukabiliana nalo. Huu si wakati wa kubuni sakata za ufisadi zisizokuwepo,” aliisema.

kwa lengo la kulipiza kisasi kwa masuala yasiyo na msingi,” akasema.

Bunge la kaunti hiyo lilisema kwenye taarifa kwamba halitalegeza kamba katika majukumu yake ya kusimamia uongozi bora wa kaunti, na halitasita kupendekeza afisa yeyote wa kaunti aadhibiwe vikali iwapo atapatikana alifuja pesa za umma.