Habari

Gavana Twaha awafurusha mawaziri kuzima malalamishi

April 5th, 2018 2 min read

NA KALUME KAZUNGU

GAVANA wa Lamu, Fahim Twaha, Alhamisi amefanya mabadiliko makuu kwenye baraza lake la mawaziri huku mawaziri wawili wakitemwa.

Katika mabadiliko hayo, Bw Twaha alimteua Bi Anne Gathoni kuwa Waziri wa Afya, nafasi ambayo awali ilikuwa ikishikiliwa na Bw Raphael Munyua.

Gavana Twaha pia alimteua Bw Paul Kamau Thairu kuwa Waziri wa Kilimo na Maji katika nafasi hiyo iliyokuwa ikishikiliwa na Bi Florence Ndung’u.

Wakati huo huo, Bw Twaha alimteua Dkt Abubakar Badawy kuwa afisa mkuu katika Idara ya Afya na Matibabu ya umma.

Pia alimteua Bi Farida Abdullahi Hassan kuwa Afisa Mkuu katika Idara ya Masuala ya Bajeti ilhali Bw John Mburu ambaye awali alikuwa ameteuliwa kutwaa wadhfa huo akitemwa.

Maafisa wote walioteuliwa na Gavana Twaha watapitia shughuli ya kupigwa msasa na bunge kabla ya watakaopasi kuidhinishwa kuhudumia idara zao.

Kwingineko, Bunge la Kaunti ya Lamu limepewa idhini ya mahakama inayowaruhusu kuendelea kuwapiga msasa maafisa wanne wa idara mbalimbali katika kaunti hiyo.

Bw Raphael Munyua ambaye alikuwa Waziri wa Afya na Mazingira kabla ya kutemwa kwenye baraza la mawaziri na gavana Twaha. Picha/ Kalume Kazungu

Awali, mahakama kuu ya Malindi ilikuwa imetoa agizo la kusitisha shughuli ya bunge hilo ya kuwapiga msasa maafisa hao, akiwemo Bi Aisha Muchile (fedha), Bi Fatma Said Abdalla (kilimo), Bw Kuria Joseph Ng’ang’a (Masuala ya Vijana) na Bw Said Mohamed Bwanamkuu (Usaidizi wa Afya, Mazingira na Usafi).

Mawasiliano hayo kati ya Bunge na Mahakama yalisomwa na Spika wa Bunge la Kaunti ya Lamu, Bw Abdul Kassim Ahmed.

“Nimepokea mawasiliano ya korti kwamba agizo la mahakama la kusitisha upigwaji msasa wa maafisa wanne wa idara za kaunti kwa sasa halipo tena.

Bunge limeruhusiwa kuendelea na upigaji msasa wa maafisa hao ambao majina yao tayari ninayawasilisha kwa kamati husika ya upigaji msasa bungeni,” akasema Bw Kassim.

Aidha hatima ya maafisa waliotemwa baada ya gavana kutekeleza uteuzi na mageuzi hayo mapya haijajulikana.

Kutemwa kwa Bw Munyua kutoka kwa idara ya afya kunajiri wakati ambapo wahudumu wa afya eneo hilo wamekuwa wakishiriki maandamano ya mara kwa mara kumlalamikia afisa huyo kwa kile wanachodai kuwa ni kuwakadnamiza, kuwahamisha ovyo ovyo kwa lazima na pia vitisho vya mara kwa mara kutoka kwa waziri huyo kwamba angewafuta kazi.