Habari Mseto

Gavana wa Bomet akaangwa na maseneta kwa kukiuka sheria ya uajiri

September 9th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

MASENETA wamempa Gavana wa Bomet Hillary Barchok makataa ya wiki mbili kuelezea kile anachofanya kurekebisha ukiukaji wa sheria inayohitaji serikali za kaunti kuajiri asilimia 30 ya wafanyakazi kutoka nje ya kaunti husika.

Hii ni baada ya ripoti Mkaguzi Mkuu wa Hesaba za Serikali ya mwaka wa kifedha wa 2017/2018 kusema kuwa kati ya wafanyakazi 3,924 waliokuwa katika sajili ya wafanyakazi wa kaunti hiyo, wakati huo, jumla ya 2,968 wanatoka Bomet.

Idadi hii, ripoti hiyo ikasema, ni sawa na asilimia 95 ya idadi jumla ya wafanyakazi waliokuwa wameajiriwa na serikali hiyo wakati ukaguzi huo ulifanyika. Hii ina maana kuwa serikali ya Kaunti ya Bomet ilikuwa imeajiri asilimia tano pekee ya wafanyakazi kutoka nje ya kaunti hiyo.

“Hii ni kinyume cha Sura ya 10 ya Katiba na Kipengele cha 65 (c) cha sheria ya Serikali za Kaunti inahitaji kwamba asilimia 30 kutoka nje ya Kaunti husika,” ikasema ripoti hiyo ambayo ilikuwa ikichambuliwa na Kamati ya Seneti kuhusu Uhasibu na Uwekazaji (CPAIC) Jumatano katika majengo ya bunge.

Mwenyekiti wa kamati hiyo Profesa Sam Ongeri alimlaumu Gavana Barchok kwa kuhusu hali kama hiyo ya ukiukaji wa sheria kutokea katika kaunti ya Bomet.

“Nakupa muda wa wiki mbili uwasilishe taarifa mbele ya kamati hii ukionyesha hatua ambazo umechukua kufikia sasa kurekebisha hali hiyo ya ukiukaji sheria. Ugatuzi haukianzishwa nchini kuepalilia ukabila kupitia uajiri,” akasema Ongeri ambaye ni Seneta wa Kisii.

Nao maseneta Johnnes Mwaruma (Taita Taveta), Samson Cherargei (Nandi) na Ochilo Ayacko (Migori) pia walimtaka mkuu huyo wa kaunti ya Bomet kuhakikisha kuwa serikali inafuata sheria ya uajiri.

Akijitetea, Gavana Barchok alielekeza lawama kwa utawala wa gavana wa zamani Isaac Ruto akisema wengi wa wafanyakazi hao waliajiri wakati wake. Bw Ruto ambaye ni kiongozi wa Chama cha Mashinani (CCM) alibwagwa na marehemu Joyce Laboso katika uchaguzi wa 2017.

“Mimi na marehemu Joyce Laboso tulirithi wafanyakazi hao kutoka serikali ya awali ya Bw Isaac Ruto. Gavana huyo wa zamani ndiye alikiuka sheria za uajiri kwa kukosa kuajiri idadi tosha ya wafanyakazi kutoka nje ya Bomet,” akasema.

“Hata hivyo tangu wakati huo, tumekuwa tukitoa nafasi kwa watu kutoka kaunti zingine nchi ya Bomet. Kwa mfano, juzi tuliajiri madaktari wanne na watatu kati yao walitoa kaunti zingine. Binafsi katika afisi yangu, nimeajiri watu wawili kutoka jamii zingine za nje,” akaongeza.

Gavana huyo aliwahikikisha maseneta hao kwamba anafanya juu chini kuhakikisha kuwa serikali inaendesha uajiri kwa kulingana na Katiba pamoja na sheria husika.