Habari Mseto

Gavana Wa Iria afufua pendekezo Nairobi ilipie maji kutoka Murang'a

August 28th, 2019 2 min read

Na NDUNGU GACHANE na MARY WANGARI

SIASA za Kaunti ya Murang’a zimechukua mkondo usiotarajiwa huku Gavana Mwangi wa Iria akifufua tena pendekezo la kutoza ada maji yanayosambazwa Nairobi na pia kumtaka afisa anayesimamia idara ya maji kaunti yake, Joseph Irungu ajiuzulu.

Akizungumza Jumatano, Wa Iria ametishia kumshtaki Bw Irungu kwa madai ya kuwazuia watu wa Murang’a kunufaika kutokana na mapato yanayopatikana baada ya maji hayo kusambazwa jijini Nairobi.

Gavana huyo amesema kwamba, huku wakazi wa Nairobi wakinufaika kutokana na maji, watu wa Murang’a wanapaswa vilevile kunufaika kwa njia iyo hiyo la sivyo wapate mapato kutokana na maji yanayotolewa kaunti hiyo.

Aidha, Bw Iria amemshutumu Katibu huyo dhidi ya kuingiza siasa katika miradi mingineyo ya maji inayoendelezwa Muranga kwa lengo la azma yake ya kuwania ugavana 2022 akimtaka ajiuzulu na kujihusisha kikamilifu na siasa za eneo hilo.

Kulingana na kiongozi huyo wa kaunti, afisa huyo amekuwa akizunguka kote katika kaunti hiyo kwa kisingizio cha kuzindua miradi ambayo tayari imekuwepo huku ‘akiwahadaa’ wakazi kwamba ni yeye amepigia debe kuanzishwa kwa miradi hiyo, akisisitiza kwamba atakuwa akihudhuria mikutano iyo hiyo kuwaeleza watu “ukweli.”

“Bw Wairagu anazunguka kote katika kaunti akizindua miradi ya maji ambayo tayari inaendelea na kujifanya kuanzisha mingine ambayo ilianzishwa hata kabla hajachaguliwa kama Katibu. Nimepania kumkomesha na nitakuwa nikihudhuria mikutano ambayo atakuwa akienda ili kuwaeleza watu ukweli,” amesema.

“Ninamwambia ajiuzulu ili azunguke kaunti yote akiwa na lengo wazi la kufanya kampeni kwa sababu anakiuka amri ya Rais Uhuru Kenyatta, hii ni miradi iliyotengewa uzinduzi na kuanzishwa rasmi na Kiongozi wa Taifa lakini anakamua kwa kutumia nyasi ya watu wengine,” alisema.

“Acha ajue nitaunda jukwaa tambarare kwa kampeni za ugavana 2022 na sitaacha awakanganye wapiga kura,” alisema.

Hata hivyo, Katibu huyo ameahidi kuendelea kukagua na kuzindua miradi huku akiamua kutojibu madai hayo ya gavana.

“Nitaendelea kukagua na kuzindua miradi katika kaunti ya Murang’a jinsi nimekuwa nikifanya kila mara,” amesema kupitia ujumbe mfupi.

Gavana na Katibu wanaotoka kijiji kimoja cha Kiharu waligeuka kuwa mahasimu wakuu baada ya Bw Wa Iria kumshutumu Bw Irungu dhidi ya kujaribu kutatiza azma yake ya kugombea ugavana 2017 pamoja na kutumia nafasi yake kuwakamata na kuwatishia wafuasi wa gavana.