Habari Mseto

Gavana Wa Iria avuta pumzi korti ikitoa agizo kuzuia yeye kukamatwa

November 23rd, 2020 1 min read

Na JOSEPH WANGUI

GAVANA wa Kaunti ya Murang’a Mwangi wa Iria amepata afueni baada ya mahakama kutoa agizo la kuzuia kukamatwa kwake, kwa kukaidi amri ya kufika mbele ya kamati ya Seneti kuwajibikia matumizi ya fedha katika serikali yake.

Kwenye agizo lililotolewa na Jaji Kanyi Kimondo, mahakama kuu pia imezuia polisi kuingilia uhuru wa Bw Wa Iria kuhusiana na amri za kumtaka afike mbele ya Kamati ya Seneti kuhusu Uhasibu na Uwekezaji (CPAIC), kujibu maswali yaliyoibuliwa kwenye ripoti za mkaguzi wa hesabu za serikali.

Jaji Kimondo alitoa agizo hilo baada ya Gavana kwenda kortini kupinga barua iliyoandikwa na CPAIC kwa Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai, ikimtaka amkamate Bw Wa Iria kwa kukaidi amri ya kufika mbele yake.

Katika uamuzi, Jaji Kimondo alisema uamuzi wa kamati hiyo, inayoongozwa na Seneta wa Kisii Sam Ongeri, kuamuru Wa Iria akamatwe ni kinyume cha sheria.

Hii, kulingana na Jaji huyo, ni kwa sababu Gavana huyo hakupewa nafasi ya kujitetea.