Habari Mseto

Gavana wa Kiambu awajali wagonjwa

May 4th, 2020 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

WAGONJWA wote waliokwama nyumbani katika Kaunti ya Kiambu na hasa wakongwe watapelekwa hospitalini na kutibiwa bure.

Gavana wa Kiambu Dkt James Nyoro alisema imebainika ya kwamba kuna wagonjwa wengi waliokwama nyumbani mwao kwa sababu hawana uwezo wa kwenda kutibiwa.

“Tutafanya juhudi kuona ya kwamba hakuna mgonjwa yeyote anayeathirika nyumbani bila kupata matibabu,” alisema Dkt Nyoro.

Aliyasema hayo mnamo wikendi katika kijiji cha Kiandutu mjini Thika, ambapo wakongwe na walioathirika zaidi ya 400 walinufaika na chakula.

Alisema tayari amepata malilio ya wakazi wa eneo hilo na cha muhimu kwa sasa ni kusambaza chakula, maji kwa wingi, na kudumisha usafi.

“Nitazungumza na kampuni ya maji ya Thiwasco water Company kuona maji yanasambazwa kwa wingi katika kijiji hicho,” alisema Dkt Nyoro.

Alisema atafanya juhudi kuona ya kwamba wakazi wote wa Kiandutu wanapewa barakoa za bure ili kujikinga na homa ya Corona.

Alisema kwa muda wa siku chache zijazo maafisa wa afya wataanza zoezi la kupima watu homa ya Corona ili kupambana na janga hilo.

Alisema tayari kaunti ya Kiambu imepata chakula kinachoweza kutosha wengi lakini alisema atataka kupata orodha kamili ya wanaohitaji msaada huo.

“Iwapo tutapata orodha kamili ya watu wanaotaka chakula bila shaka kila mmoja atanufaika,” alisema Dkt Nyoro.

Alisema hakuna baa yoyote itaruhusiwa kwa vyovyote vile kufunguliwa hadi swala la corona liangamizwe.

Alihimiza wakazi hao wadumishe usafi wa hali ya juu ili kukabiliana na janga hilo.

Alisema kijiji cha Kiandutu kina wakazi wengi wanahitaji msaada na kwa hivyo angetaka kupata idadi kamili ya watu hao ndipo kuwe na mikakati maalum ya kuwasaidia.

 

Kiongozi wa vijana katika kijiji hicho Bw Stanley ‘Stano’ Njuguna, alisema kuna wagonjwa wengi wanaohitaji msaada wa kimatibabu.

“Hapa Kiandutu watu wanapitia shida nyingi ajabu na kwa hivyo tunataka Kaunti ya Kiambu iingilie kati ili wapate usaidizi,” alisema Bw Njuguna.

Alisema kijiji hicho kina wakazi zaidi ya 20,000 na kwa hivyo wanahitaji usaidizi wa dharura.

Bw Peter Kimani ambaye ni kijana wa kijiji hicho alisema wao kama vijana wachache wamejitolea kwa kusaidia wakongwe kwa kuwachotea maji bila malipo yoyote.

Alitoa mwito kwa gavana kuona ya kwamba vijana wanapata usaidizi wa ajira ili wajikimu kimaisha.