Habari za Kaunti

Gavana Wavinya apiga marufuku maiti za ‘wageni’ kupelekwa Machakos

January 7th, 2024 1 min read

NA MWANGI MUIRURI 

GAVANA wa Machakos Bi Wavinya Ndeti ametoa amri kwa wahudumu wa mochari za eneo hilo kukoma kupokea maiti za wageni.

Mkuu huyo wa kaunti amesema mochari za Machakos zinashuhudia ongezeko la miili hasa kutoka nje ya kaunti, jambo ambalo linatatiza wakazi.

Kwa mfano, anasema hospitali kuu ya Machakos imeathirika pakubwa kwa sababu makafani yake hayana uwezo kuhifadhi maiti nyingi.

Ina nafasi ya miili 24 pekee, na Bi Wavinya anasema ikipokea zaidi ya idadi hiyo huenda huduma zake zikatatizika.

“Hospitali hii ina miili 62 ambayo imejaa hapa bila wenyewe kuja kuitambua. Ndio sababu Gavana sasa ametoa amri kwamba tuwe tukipokea miili ya wenyeji pekee,” akasema Waziri wa Afya Machakos, Bw Daniel Yumbya.

Bw Yumbya aliongeza kwamba “polisi ambao huokota miili kutoka ajali na vichaka katika Kaunti za Kajiado, Nairobi, Makueni, Kiambu…Wasiwe wanaileta hapa…Muwe tu mnaleta miili ambayo mumeokota kutoka hapa kwetu Machakos”.

Waziri huyo wa afya katika kaunti alisema kwamba msongamano wa miili katika Mochari ya Machakos umefanya uhifadhi wa maiti za wenyeji kuwa ngumu.

“Hili linafaa liwafikie maafisa wa polisi kwa kuwa ndio kiini cha changamoto hii…Hatutapokea miili ambayo mumeokota nje ya kaunti hii,” akasema.

[email protected]