Habari Mseto

Gazeti la Taifa Leo lachupa hadi nafasi ya 3 kwa usomaji

August 12th, 2019 1 min read

NA MWANDISHI WETU

GAZETI la Taifa Leo limeibuka kuwa mojawapo wa magazeti matatu yanayosomwa na watu wengi zaidi nchini, huku likiyapiku magazeti ya The Star, People Daily, The Nairobian, Saturday Standard na Sunday Standard.

Kulingana na utafiti wa majuzi uliofanywa na shirika la Kenya Audience Research Foundation (KARF), gazeti la Taifa Leo, ambalo ndilo la pekee la kila siku linalochapishwa kwa Kiswahili, ni nambari tatu kwa kusomwa na Wakenya wengi kutoka kila pembe ya nchi.

Gazeti la Daily Nation, ambalo sawa na Taifa Leo huchapishwa na kampuni ya Nation Media Group, ndilo linaloongoza kwa kusomwa na watu wengi nchini, likifuatwa na Standard.

Taifa Leo, ambalo limekuwa likichapishwa kwa miaka 61, limekuwa sehemu ya historia ya Kenya kwa kunakili matukio muhimu tangu harakati za kupigania uhuru pamoja na kutetea haki za wanyonge na uadilifu.

Pia limeendelea kudumisha heshima yake ya kutopendelea upande wowote na kuchapisha habari na makala yenye manufaa kwa jamii.

Katika miaka ya majuzi Taifa Leo limetambulika katika shule za msingi na sekondari kama kifaa muhimu katika kuimarisha somo la Kiswahili.

Utafiti huo ulifanyika katika miezi ya Februri na Machi 2019.

Hii hapa orodha kamili:

1. Daily Nation 48.3%
2. The Standard 25.3%
3. Taifa Leo 6.0%
4. Sunday Nation 5.6%
5. Saturday Nation 5.6%
6. People Daily 2.7%
7. Saturday Standard 2.5%
8. Sunday Standard 2.3%
9. The Nairobian 2.3%
10. Mwanaspoti 1.8%
11. The Star 1.2%
12. Mengine N/A

Chanzo: KARF