Habari za Kitaifa

Gen Z wahangaisha polisi wakiandamana kupinga Mswada wa Fedha 2024


JIJI LA NAIROBI Jumanne liligeuka kuwa uwanja wa vita polisi na waandamanaji walipokabiliana vikali kuhusu Mswada wa Fedha 2024 .

Licha ya polisi kusema maandamano hayo yalikuwa haramu vijana na makundi mbalimbali yajibwaga barabarani kuonyesha pingamizi zao.

Shughuli jijini jana zilisimama huku waandamanaji wakipiga nduru na kukemea uongozi wa Rais William Ruto, wakilalamikia ushuru mwingi ambao wamelimbikiziwa.

Maandamano hayo yaliyofahamika kama ‘Occupy Parliament (Keti Bungeni) yalikuwa yakilenga kuwaonya wabunge wasipitishe mswada huo tata. Kati ya wale ambao walikamatwa ni mwanaharakati na mwanahabari Hanifa Adan ambaye alikuwa akiandamana karibu na mnara wa Tom Mboya.

Polisi, baadhi wakiwa wamevalia nguo za raia, waliwanyaka na kuwatia pingu waandamanaji waliovalia mashati yao meusi

“Mtatukamata wote,” akasema mwendeshaji wa pikipiki akiwa Moi Avenue huku pamoja na wenzake wakiwazomea polisi waliokuwa wanawaweka waandamanaji katika karandiga lao.

Mara ya mwisho ambapo Nairobi ilishuhudia maandamano kama jana ni mwaka jana, wakati ambapo Kinara wa Upinzani Raila Odinga aliyaitisha.

Barabara ya kuelekea bunge karibu na afisi za Hazina ya Fedha nazo hazikuwa zikipitika huku polisi wakiwa ange kuwakabili waaandamanaji.

Hata katika barabara za Ronald Ngala, Muthurwa, Koja na Hailesallasie ambazo zipo nje ya jiji kidogo, biashara zilikuwa zikiendelea japo kulikuwa na taharuki.

Wafanyabiashara katika soko la Muthurwa waliunga maandamano hayo wakimrejelea Rais kama kiongozi msaliti ambaye sera zake za kiuchumi zimesambaratisha biashara zao.

“Huo mswada ni mbaya. Ruto ni mwongo na hayo mabadiliko wanayoyasema ni kutuhadaa tu,” akasema mfanyabiashara Martha Wairumu. Wengi waliokamatwa jana walipelekwa katika seli za kituo cha polisi cha Central.

Kamatakamata hizo zilishamiri nje ya jumba la Nation, Tom Mboya, Aghakan Walk, Moi Avenue, Uhuru Highway na barabara ya Parliament. Jiji lilikuwa kama mahame, milio ya risasi na gesi za kutoa watu machozi zilitanda kila mahali.

Wengi waliyaacha magari yao nyumbani wakihofia usalama wao nao polisi waliojihami vikali wakionekana kutibua makundi ya watu waliokuwa wakijikusanya maeneo mbalimbali.