Habari Mseto

Genge hatari linalolawiti walevi kabla ya kuwaua lazua hofu Murang’a

December 16th, 2019 1 min read

Na NDUNGU GACHANE

GENGE la wahalifu ambao wamekuwa wakilawiti wanaume, haswa walevi, katika vijiji vya Gakoigo, Nyakagumo na Ihigaini, eneobunge la Maragua, Kaunti Murang’a limezua hofu huku wengi wa walevi wakilazimika kurejea nyumbani kabla ya jua kutua.

Wahalifu hao wanalenga wanaume wa umri wa miaka 40 na zaidi.

Wiki iliyopita, Julius Njoroge Mburu, 40, alilawitiwa na kisha kuuawa na genge hilo.

Baada ya kutekeleza mauaji hayo, wahalifu hao walichoma shingo la mwendazake na kisha kuficha mwili wake kichakani, kilomita chache kutoka mjini Gakoigo.

Inashukiwa kwamba Mburu aliuawa kabla ya saa tano usiku, kulinganana na wenzake aliokuwa akibugia nao pombe.

Ndugu ya mwendazake, Moses Kamande Mburu, alisema kuwa nduguye alienda kunywa pombe Jumamosi, wiki iliyopita, lakini hakurejea nyumbani.

“Siku iliyofuatia tulifahamishwa kuwa mwili wake ulipatikana kichakani takriban kilomita moja kutoka nyumbani,” akaambia Taifa Leo.

“Nilipofika katika eneo la tukio nilipata ndugu yangu akiwa uchi na amenyongwa kwa waya,” akaongeza.

Hayo yalijiri baada ya mwanaume mwingine kulawitiwa na kuuawa na genge hilo karibu na soko la Gakoigo.

Mama ya mwendazake, Teresiah Njeri, alisema kuwa polisi hawajakamata yeyote kuhusiana na mauaji hayo ya mwanawe.

Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Murang’a, Josphat Kinyua aliambia Taifa Leo kuwa wanaendelea na uchunguzi kwa lengo la kunasa wahalifu hao.

“Maafisa wa polisi wametumwa katika vijiji hivyo kufuatilia wahalifu matukio hayo,” akasema.

Visa hivyo sasa vinalazimu wakazi kwenda nyumbani kabla jua halijaingia.