Habari Mseto

Genge la ‘Gaza’ lamuua mwanajeshi aliyekataa kuwapa Sh60

February 8th, 2019 1 min read

NA NDUNGU GACHANE

MWANAJESHI wa zamani, Jumatano aliuawa na wanachama wa kundi hatari la Gaza linalowahangaisha wananchi wa Kiharu, Kaunti ya Murang’a baada ya kukataa kuwapa Sh60.

Samson Kamau, 65, alikuwa akihesabu fedha zake alipovamiwa na wanachama wa Gaza waliomtaka awakabidhi pesa hizo ila akakataa ndipo wakamdunga kisu hadi akafa.

Mkewe, Bi Margaret Wambui Kamau alisema alimweleza mumewe aliyetoka nyumbani saa 10 jioni arudi nyumbani mapema kutokana na kukithiri kwa utovu wa usalama ila akavamiwa na wanachama watano wa kundi la Gaza waliomzingira na kumuua alipokuwa akitaka kupanda pikipiki ya kumleta nyumbani.

“Wanne walikimbia lakini mmoja aliyeshikwa na wenyeji alifichua majina ya wenziwe na kusimulia jinsi wamekuwa wakitumia nyundo na visu kuwavamia wanakijiji,” akasema Bi Kamau.

Bintiye marehemu, Jane Wairimu naye alisimulia jinsi kundi hilo lilivyoteka vijiji vya Mukuyu, Mjini, Mumbi na Maragi wanakoibia na kuwajeruhi wenyeji na wafanyabiashara bila huruma.

“Mwaka jana kundi hilo lilimuandama mume wangu na kumuibia simu na pesa taslimu kisha wakampiga hadi akapoteza fahamu. Walifanya hayo ndani ya nyumba yetu na hata kilio changu hakikuweza kuwakomesha. Walitutisha kwamba wangetuua iwapo tungepiga kelele,” akasimulia Bi Wairimu.

Hata hivyo, Kamanda wa polisi wa kaunti ya Murang’a Mohammed Farah alilalamika kwamba juhudi za maafisa wake kuwamaliza wanachama wa Gaza zimekuwa zikitatizwa na mahakama ambayo huwaachilia washukiwa kutokana na ukosefu wa ushahidi kila mara.

Mwaka jana wanachama 12 wa Gaza waliofikishwa katika mahakama ya Murang’a waliachiliwa huru baada ya ushahidi kukosekana.

“Tumemkamata mshukiwa moja kutokana na mauaji haya na bado tunawasaka wengine. Tutazidisha doria,” Bw Faraha akaambia TaifaLeo.