Habari

Genge laiba ng'ombe 8 na kuwachinja kwa mochari

June 12th, 2018 2 min read

NA PETER MBURU

POLISI mjini Nakuru wanawawinda genge la majambazi ambalo usiku wa kuamkia Jumanne liliiba ng’ombe wanane kutoka shamba la mkulima mmoja na kuwachinja karibu na mochari.

Wezi hao wanasemekana kuvamia shamba la Bi Damaris Njeri, mtaa wa East Gate, Pipeline mwendo wa saa kumi usiku wakiwa wamejihami na mapanga, kabla ya kuondoka na mifugo hao aina ya Friesian.

Sehemu za ngombe zilizosalia kama idhibati baada ya wezi kuiba na kuwachinja kando ya chumba cha kuhifadhi maiti cha Umash, Nakuru Juni 12, 2018. Picha/ Peter Mburu

“Nilipigiwa simu saa kumi alfajiri na mfanyakazi wangu wa shambani na akanieleza kuwa wezi wamewavamia na wakaiba ngombe wote wa maziwa. Baadaye nilimpigia chifu wa eneo hilo ambaye aliahidi kufahamisha polisi,” akasema Bi Njeri.

Mwanamke huyo alieleza Taifa Leo kuwa baada ya saa mbili alifika kwenye kituo cha polisi cha Mwariki kuripoti, ijapokuwa mkuu wa polisi kituo hicho alidai ‘kuwekewa mafuta’ kwenye gari la kazi kabla ya kwenda kutafuta mifugo hao.

Kichwa cha mmoja wa ngo’mbe walioibwa na kuchinjwa karibu na mochari Nakuru. Picha/ Peter Mburu

“Nilipopiga ripoti mwendo wa saa kumi na mbili, Bw OCS alinitaka kutoa Sh1,000 akisema ni za kuweka gari la polisi mafuta, ilinibidi nitoe kwani nilihitaji msaada wao,” akasema mwanamke huyo.

Mkulima huyo alieleza ghadhabu yake na tabia ya polisi hao, ambao hawawezi kuwasaidia wananchi kabla ya kupewa rushwa.

“Si vyema hata kidogo kuwa ili kuhudumiwa na polisi wananchi wanahitajika kuwahonga kwanza. Huenda hii ndiyo sababu visa vya wizi vimezidi katika mtaa huu,” Bi Njeri akasema.

Kichwa na ngozi zilizosalia baada ya wezi kubeba nyama. Picha/ Peter Mburu

Naibu wa OCPD Nakuru Bw Daniel Kitavi alisema hakuna takwa lolote katika huduma za polisi linalohitaji wananchi kulipia gharama za kusaidiwa kuweka ulinzi na polisi.

“Siku hizi, magari ya polisi yanawekwa mafuta kwa kutumia kadi wala si pesa taslimu, ikiwa afisa huyo aliitisha pesa, hicho ni kinyume cha maadili na sharia na atachukuliwa hatua za kisheria,” akasema Bw Kitavi.

Kinaya cha yote kilikuwa, baada ya ‘kupokea pesa za mafuta’ polisi hawakufanikiwa kuwapata mifugo hao kwani walipata baadhji ya sehemu za mizoga yao, baada ya kuchinjwa na wezi kuondoka na nyama.

Mguu na ngozi zilizopatikana katika eneo ambapo ng’ombe walichinjwa. Picha/ Peter Mburu

Wezi hao waliwachinjia ngombe wa mkulima huyo kando ya chumba cha kuhifadhi maiti cha Umash, lakini hawakubeba vichwa, kwato na ngozi.

“Ngombe wote walikuwa wamechinjwa, tulipata vichwa, ngozi na kwato pekee lakini nyama zilikuwa zimebebwa,” akasema Bi Njeri.

Hadi wakati wa kuandika taarifa hii, hakuna mwizi aliyekuwa amekamatwa na polisi.