Genge linavyohangaisha wanawake na wasichana

Genge linavyohangaisha wanawake na wasichana

NA WAIKWA MAINA

WAHALIFU sugu wenye silaha kali na hatari ambao wanalenga akina mama na wasichana wadogo, wamevamia kaunti ya Nyandarua, na kusababisha mauaji, ubakaji kisha kuwaacha waathiriwa na makovu ya kudumu maishani.

Genge hilo la wahalifu halionekani kutetereka licha ya onyo kali kutoka kwa wakuu wa polisi ambao sasa wamelazimika kutembelea maeneo ambayo mauaji yametokea, kuandaa vikao na wanahabari, kuwapeleka majeruhi hospitalini na kuwaarifu wakubwa wao kuhusu matukio mbalimbali.

Maeneobunge ya Ol Joro Orok na Ol Kalou ndiyo yameathirika zaidi na hili lilidhihirika Ijumaa wiki jana ambapo Bi Mary Nyambura, mfanyakazi wa serikali ya kaunti ya Nyandarua alibakwa na magenge hayo kisha akauawa kinyama.

Majuma mawili yaliyopita, msichana mwenye umri wa miaka 14 alibakwa na kuachwa akiwa hali mahututi kwenye kaburi la babake huku mwanaume mwengine akikatwa kwa panga na kuuawa alipoenda kumwokoa msichana mdogo aliyekuwa akibakwa na genge jingine la wahalifu.

Katika eneobunge la Ol Kalou, Bw Michael Mathenge na mpenziwe Mary Wanjiku waliuawa mwezi Oktoba huku Bi Rose Wanjiku akipigwa kibuhuti na wahalifu na bado anaendelea kutibiwa katika hospitali ya Nakuru akiwa na majeraha mabaya.

Kwenye kisa cha Ol Joro Orok, Bi Nyambura alibakwa na kuchinjwa kilomita chache tu kutoka nyumbani kwake ambapo Kamanda moja wa polisi wa utawala pia anaishi.

Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Nyandarua Gideon Ngumi alisema mwili wa marehemu ulikuwa na majeraha mabaya kichwani na kukatwa kwenye shingo na polisi wanaamini kwamba alibakwa kabla ya mauaji hayo.

Bi Nyambura,47 ambaye alikuwa akielekea nyumbani kwake kutoka Nairobi alipokumbana na mauti hayo huku mwili wake ukipatikana Jumamosi asubuhi na wapita njia.

Ni kutokana na visa hivi ambapo Gavana wa Nyandarua Francis Kimemia ametoa wito kwa uchunguzi wa kina kuendeshwa huku akionyesha kukerwa kwake na mauaji hayo yanayotokea wakati wa kuadhimishwa kwa siku ya kimataifa ya Kutokomezwa kwa Dhuluma na Ghasia dhidi ya Wanawake.

“Kifo cha Bi Nyambura kinasikitisha na kinaibua uchungu mwingi.

Kinaonyesha kwamba kila moja wetu anafaa kusimama wima na kupinga dhuluma dhidi ya wanawake,” akasema Bw Kimemia.

You can share this post!

Demu mlevi atimua wazazi

EACC yatofautiana na polisi kuhusu ufyatulianaji risasi na...

adminleo