Makala

GEORGE MUNYUA: Nimeshirikiana na wasanii zaidi ya 100

November 22nd, 2019 2 min read

Na JOHN KIMWERE

SAFARI ndefu huanza kwa hatua moja. Ndivyo anavyosadiki msanii chipukizi anayepania kufanya kweli kama prodyuza wa nyimbo za kizazi kipya hapa nchini.

Analenga kujitambulisha katika ulingo wa burudani ya muziki na kuutikisa sawasawa bila kulaza damu. Katika mpango mzima, George Ng’ang’a Munyua anataka kujituma mithili ya mchwa bila kupunguza spidi huku akilenga kufikia hadhi ya prodyuza wa kimataifa miaka ijayo. ‘

‘Ninaamini hakuna kisichowezekana ingawa ndiyo nimeanza kusukuma gurudumu katika masuala ya kurekodi muziki ambapo ninajihisi nina talanta ya kufanya kweli,” alisema chipukizi huyu ambaye kisanaa anafahamika kama Purple G Beats.

Chipukizi huyu anamiliki studio iitwayo Purple G Beats Lab inayopatikana katika mtaa wa Umoja One Section C katika Kaunti ya Nairobi iliyozaliwa mwaka jana (2018).

”Hakika safari yangu ni ndefu sio mzaha ambapo kama prodyuza nina rekodi nyimbo za densi vile vile kumtukuza Mungu tena kwa mitindo mbali mbali ikiwamo Hip Hop, rap, dancehall, reggae bila kuweka katika kaburi la sahau bongo fleva,” anasema na kuongeza kuwa kama produsa amejitwika jukumu la kutengeneza midundo (beats) ya nyimbo tofauti na kuwauzia wanamuziki wanokuja.

Anasema baada ya kuzitengeneza uzitupia katika mtandao ya Youtube kwenye jitihada za kutafuta wateja.

Kimsingi anasema ni vizuri msanii kuwa mbunifu katika taaluma yake pia kutia bidii na kumtegemea Muumba ili kufanikisha maazimio yake. Picha/ John Kimwere

Anadokeza kuwa tangu aanzishe studio hiyo amefanikiwa kufanya kazi na wasanii zaidi ya 100, baadhi yao wakiwa: Dash Jay (nyimbo Savage), Polo G (Pamba), Reckless (Panda Freestyle), Naomi (In the Streets), Niniola (Mapenzi ni dawa) na Arrow Boy (African Queen).

Msanii huyu anadokeza kuwa hana la ziada ila anajituma kiume anakolenga kufikia kiwango cha maprodyuza mahiri duniani kama Jayna na Wondagurl raia bara Ulaya na Canada mtawalia. Hapa nchini anasema amepania kufuata nyayo zao Magix Enga na Motif the Beats Don.

Kabla ageukie taaluma ya produsa za amekuwa akighani nyimbo za kizazi kipya kwa mtindo wa rap ambapo kwa sasa anajivunia kuwa katika masuala ya muziki ndani ya miaka mitano.

Anajivunia kutunga na kutoa nyimbo nyingi tu ikiwamo ‘Nimefyatua kiasi,’ ‘Chance,’ ‘Koo Bobo,’ ‘Ukisema wanipenda,’ na ‘Rangi ya Thao.’

”Kenya ina wanamuziki wengi tu ambao mara nyingi hujinyima usingizi wakati wengine wamelala ili kufanya utafiti kuhusu namna ya kujiendeleza kusudi kupeperusha bendera ya taifa hili katika muziki,” alisema na kuongeza kuwa anajivunia kuwa miongoni mwao.

Kijana huyu anaitaka serikali kuwa makini zaidi kwenye mkakati wa kulinda haki za wasanii ili wafaidi kwa jasho lao badala ya kuendelea kunyonywa na wafanyi biashara wajanja wa muziki ghushi.

Anaamini serikali ikiweka juhudi mwafaka na kuzima matapeli muziki wa Kenya hutapata nafasi nzuri ya kutamba.