Habari Mseto

Gereza la Shimo la Tewa lamtaka mahabusu Sonko

November 24th, 2019 2 min read

Na MWANDISHI WETU

WAKUU wa gereza la Shimo la Tewa, sasa wanamtaka Gavana wa Nairobi Mike Mbuvi Sonko kutumikia kifungo ambacho hakukamilisha baada ya kutoroka kutoka gereza hilo lenye ulinzi mkali.

Kulingana na stakabadhi zilizowasilishwa mahakamani Nairobi na usimamizi wa gereza hilo lililoko Kaunti ya Mombasa, pia wanapendekeza Bw Sonko, ambaye alijulikana kama Mbuvi Gidion Kioko, ashtakiwe upya kwa kosa la kutoroka jela.

“Mfungwa kwa jina Mbuvi Gidion Kioko anahitajika ili akamilishe kifungo chake ambacho kilisalia. Vilevile, ashtakiwe upya kwa hatia ya kutoroka gerezani,” wasimamizi wa gereza la Shimo la Tewa wanasema katika stakabadhi zilizowasilishwa kwa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC).

Tume hiyo inamchunguza gavana Sonko kwa tuhuma za kuwasilisha stakabadhi zenye maelezo ya kupotosha ili aidhinishwe kuwania ugavana katika uchaguzi mkuu wa 2017.

Rekodi za mahakama zilizowasilishwa kwa EACC zinaonyesha kuwa, mnamo Machi 12, 1998, Mbuvi Gidion Kioko alihukumiwa kwa kosa la kutohudhuria vikao vya mahakama katika kesi nambari CF 675/97 na baadaye akapigwa faini ya Sh200,000.

Bw Sonko hakuweza kulipa faini hiyo na hivyo akaamuriwa atumikie kifungo cha miezi sita katika Gereza la Shimo la Tewa.

Siku hiyo hiyo, Machi 12, 1998, Sonko alipigwa faini ya Sh500,000 la sivyo asukumwe jela kwa miezi sita kwa kosa la kutohudhuria vikao vya awali vya kusikizwa kwa kesi nambari CF 1727/96.

Alihitajika kutumikia vifungo hivyo kwa muda wa miezi 12 ambapo alisajiliwa katika Gereza la Shimo la Tewa siku hiyo na akapewa nambari ya mahabusu P/No. SHO/477/1998. Sonko alipangiwa kuachiliwa huru mnamo Machi 11, 1999.

Lakini alihepa kutoka gereza hilo kiajabu, mnamo Aprili 16,1998, mwezi mmoja baada ya kufungiwa huko.

Hata hivyo, mnamo Novemba 15, 2000, afisa msimamizi wa Rumande ya Gereza la Viwandani, Nairobi, alituma ujumbe kwa gereza la Shimo la Tewa kwamba, mtu kwa jina Mbuvi Gidion Kioko alizuiliwa hapo akisubiri kushtakiwa kwa makosa mengine.

Usimamizi wa idara ya magereza ulimchukulia kuwa mfungwa hatari na kumhamisha hadi Gereza lenye ulinzi mkali la Kamiti kama mfungwa mwenye nambari KAM/1255/001s. Aliachiliwa kutoka gereza hilo mnamo Februari 12, 2001.

EACC iliwasilisha malalamishi dhidi ya gavana Sonko mnamo Septemba 19, 2019 na kuanzisha uchunguzi kivyake kufuatia habari ilizopokea kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma kuhusu rekodi ya uhalifu miaka iliyopita.

Makosa kadha

Ofisi ya DPP ilipatia EACC habari kuhusu kesi mbalimbali ambazo Sonko, akishirikiana na watu wengine, alishtakiwa kwa makosa mbalimbali ya uhalifu.

EACC ilithibitisha habari ilizopata kutoka ODPP katika vituo mbalimbali vya polisi na maafisa wa magereza na ikathibitisha kuwa habari hizo zilikuwa za kweli.

Katika stakabadhi ilizowasilisha mahakamani ikijibu kesi nambari 326 ya 2019, tume hiyo inasema imethibitisha Sonko alijaza habari za uwongo katika fomu za kuidhinishwa kuwania ugavana, akisema hajawahi kufungwa jela.

Kwa hivyo, kulingana na hati kiapo iliyoko mahakamani, Gavana alikiuka vipengee vya 13, 29 na 30 vya Sheria ya Uongozi na Maadili kwa Maafisa wa Serikali ya 2012, na hitaji la Sura ya sita ya Katiba, kwa kuwasilisha habari za uwongo kwa asasi hiyo ya umma. Pia alikosea kwa kutoa habari za kupotosha kwa Tume huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).