Habari Mseto

Gereza laeleza kwa nini limemtenga Mackenzie na wafungwa wengine

April 4th, 2024 3 min read

NA BRIAN OCHARO

IDARA ya magereza imekiri kuwa mshukiwa mkuu wa mauaji ya Shakahola, Paul Mackenzie, anatengwa na wafungwa wengine gerezani.

Kamishna Msaidizi wa gereza la Shimo La Tewa Kassim Kimuyu alieleza mahakama kuwa, mhubiri huyo ametengwa kwa vile alishtakiwa chini ya Sheria ya Kuzuia Ugaidi.

“Gereza hutumia mfumo maalumu kutathmini washukiwa au wafungwa walioshtakiwa chini ya Sheria ya Kuzuia Ugaidi. Mackenzie alitathminiwa kwa kutumia mfumo huo na kupatikana kuwa, ana uwezo mkubwa wa kuleta itikadi kali kwa wengine. Mfumo huo umethibitishwa kuwa na ufanisi katika kutathmini hatari kama hizo,” Bw Kimuyu alimweleza Hakimu Mkuu Leah Juma, mnamo Jumatano.

Bw Kimuyu pia aliwasilisha ushahidi mahakamani ambao alisema unadhihirisha wasiwasi wao kuwa Mackenzie anahusika na uenezaji wa itikadi kali akiwa gerezani.

Alionyesha daftari linalodaiwa kuwa na jumbe za itikadi kali ambazo zimeandikwa na Mackenzie.

“Hapa kuna ushahidi mmoja tu wa itikadi kali,” Bw Kimuyu alisema alipokuwa akionyesha daftari hilo mahakamani.

Alifafanua zaidi kuwa Sheria ya Magereza inaruhusu kutengwa kwa watuhumiwa au wafungwa wanaokabiliwa na mashtaka yanayohusiana na ugaidi na wale wanaoshtakiwa kwa makosa mengine.

Vilevile, mahakama iliambiwa kuwa, Mackenzie anapata fursa ya kuonana na mkewe Rhoda Mumbua Maweu kila mara.

“Wawili hao huwa wanakutana kila mara wanapotaka, ni haki yao hawawezi kunyimwa,” alisea Bw Kimuyu.

Lakini alieleza kuwa, Mackenzie huwa anatangamana na wapishi ambao pia ni wafungwa wakati wa mchana tu.

“Huko gerezani, hata Wakristo walioshtakiwa au wanaotumikia vifungo chini ya Sheria ya Kuzuia Ugaidi wanatenganishwa na wenzao Waislamu,” alisema wakati wa kuhojiwa na mawakili wa Mackenzie, Bw Wycliffe Makasembo na Bw Lawrence Obonyo.

Kuhusu madai ya njama ya kumteka nyara Mackenzie, Bw Kimuyu alisema gereza hilo lina usalama wa kutosha na hivyo basi tukio aina hiyo halijawahi kutokea.

“Hatuwezi kupuuza uwezekano wa utekaji nyara, lakini mawakili wa Mackenzie wanaweza kutoa maelezo zaidi ili kushugulikiwa na vyombo vya usalama kuhakikisha usalama wake,” alisema.

Mpelelezi Mkuu, Bw Stephen Ambani, alisema Idara ya Upelelezi wa Uhalifu (DCI) haijaanzisha uchunguzi wowote kuhusu madai ya utekaji nyara kwa vile malalamishi hayajawasilishwa kwao rasmi.

Bw Kimuyu na Bw Ambani walikuwa wakijibu madai ya Mackenzie ya kutengwa na washirika wake na yale ya njama ya kutekwa nyara.

Walitakiwa kufika mahakamani na kufafanua tuhuma hizo.

Hakimu Juma alikubaliana na maelezo yaliyotolewa na Bw Ambani na Bw Kimuyu, na kuyaona kuwa ya busara.

“Ninaona maelezo yaliyotolewa na maafisa hao wawili kuwa ya busara, mahakama haijaona ukiukwaji wowote wa haki za Mackenzie. Yeye ni mfungwa. Hata hivyo, atasindikizwa hadi kituo cha polisi kuwasilisha malalamishi yake kuhusu dai la kutekwa nyara,” alisema Hakimu.

Zaidi ya hayo, Mackenzie alipata pigo baada ya ombi la kutaka kuhamishwa kutoka gereza la Shimo La Tewa kukataliwa kwani mahakama ilisema haina mamlaka ya kukubali ombi hilo.

“Mackenzie hakufungwa na mahakama hii kwa hivyo haina mamlaka ya kuamuru ahamishwe hadi Gereza la Malindi. Mackenzie hata hivyo yuko huru kutafuta maagizo hayo katika jukwaa linalofaa,” Bi Juma alisema.

Mackenzie alitaka kuhamishwa akidai kuwa huenda amekwaza wakuu wa gereza hilo kutokana na malalmishi mengi ambayo amewasilisha mahakamani kuhusu mateso anayopitia.

Baadhi ya malalamishi yake ni pamoja na kutengwa na wafungwa wengine, kukataliwa kuota jua na malalamiko ya kupata ugonjwa wa ngozi na mengine yanayotokana na ngono.

Hata hivyo, upande wa mashtaka ukiongozwa na Bi Ogega Bosibori ulipinga ombi hilo ukisema gereza la Shimo la Tewa lina vifaa maalum vya kuwahifadhi watu wanaoshtakiwa kwa ugaidi na kuwa Mackenzie bado anakabiliwa na kesi tatu katika mahakama za Mombasa.

Mackenzie, mkewe Maweu na wengine 93 wamekana makosa manne yanayohusiana na ugaidi.

Mackenzie, Bi Maweu, Smart Mwakalama na mkewe Mary Kadzo Kahindi na wengine 28 wameshtakiwa kwa makosa ya kujihusisha na uhalifu wa kupangwa na hivyo kuhatarisha maisha na kusababisha vifo vya wafuasi wao 429.

Mackenzie, Bi Maweu, Bw Kwakalama, mkewe na wenzake 28 wanashtakiwa kwa itikadi kali, ambapo serikali ilidai kuwa washukiwa hao waliendeleza mfumo wa imani ambayo ilisababisha wafuasi wao kufunga hadi kufa.

Mackenzie na mkewe pia wameshtakiwa kwa kosa la kumiliki vifaa ambavyo vinatumika kuendeleza vitendo vya kigaidi. Vitu hivyo ni pamoja na diski, DVD na vitabu.

Serikali ilidai kuwa washukiwa hao walitenda makosa hayo katika eneo la Furunzi huko Malindi tarehe tofauti kati ya 2020 na 2023. Mahakama itatoa mwelekeo zaidi katika kesi hiyo Mei 6.