Michezo

Gerrard anasa beki wa Leicester Calvin Bassey

June 7th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

BEKI Calvin Bassey, 20, amekatiza rasmi uhusiano wake na Leicester City na kutua kambini mwa Rangers nchini Scotland baada ya kutia saini mkataba wa miaka minne.

Kikubwa zaidi kilichomfanya kuwa kivutio kwa kocha Steven Gerrard wa Rangers ni uwezo wake wa kutamba akiwajibishwa kama beki wa kati au wa kushoto.

“Klabu nyingi zilikuwa zikiwania huduma za Bassey. Ni fahari tele kwamba ni sisi tuliobahatika kumshawishi kutoelekea kokote kwingine. Ujio wake ni afueni kubwa kwa Rangers ambao watazidi kujitafutia maarifa ya chipukizi zaidi muhula huu,” akatanguliza Gerrard.

“Ni mwanasoka aliyekirimiwa ubunifu mkubwa na asiyeishiwa na pumzi kirahisi chini ya dakika 90. Mbali na uwezo wa kudhibiti mpira kwa guu la kushoto, anaweza pia kuchezeshwa kama difenda wa kati. Isitoshe, ana nguvu na kasi itakayochangia ubora wa idara ya kati uwanjani,” akasema Gerrard ambaye ni nahodha na kiungo wa zamani wa Liverpool.