Habari MsetoSiasa

Geti ya Sh20 milioni ni kosa la uchapishaji, gavana sasa ajitetea

February 22nd, 2018 1 min read

Nyeri county government headquaters in Nyeri town on February 20, 2018. The county has proposed to spend Sh20 million to contruct a new gate. BY GRACE GITAU

Na GRACE GITAU

GAVANA wa Nyeri, Bw Mutahi Kahiga, amejitetea kuwa pendekezo la kujenga lango kuu la makao makuu ya kaunti yake kwa Sh20 milioni, lilikuwa ni kasoro ya uchapishaji.

Alisema hayo huku wakazi wakilalamika pakubwa kufuatia ufichuzi huo Jumatano.

Hata hivyo, alitetea mpango wa kujenga nyumba rasmi ya gavana kwa Sh200 milioni na kusema itatumiwa pia kwa ujenzi wa nyumba ya naibu gavana.

“Ujenzi wa geti ulikamilishwa na hakuna ukarabati wowote utakaofanywa kwake. Kile kilichokuwa kwenye ripoti ya maandalizi ya bajeti kilikuwa ni kasoro ya uchapishaji,” akasema.

Geti iliyopo kwa sasa ilijengwa miaka miwili iliyopita na utawala wa aliyekuwa gavana, Bw Nderitu Gachagua.

Huku akialika wananchi kutoa maoni yao kuhusu mipango ya matumizi ya fedha Ijumaa, gavana huyo aliahidi kuhakikisha kuwa fedha za umma zitatumiwa inavyofaa.

Bw Amos Muchiri, ambaye ni mkazi wa Nyeri mjini alisema Sh20 milioni ni pesa nyingi ambazo zinaweza kusaidia kuweka lami kwa kilomita mbili ya barabara au hata kukamilisha ujenzi wa soko la Nyeri.

“Sidhani kaunti hii inahitaji ukarabati wa geti kwani ile iliyopo haina tatizo lolote. Ingawa hilo lilikuwa ni pendekezo tu na kutakuwa na uchanganuzi wa kina kabla bajeti ipitishwe, ni pendekezo lisilo na umuhimu wowote,” akasema.

Mbali na kuibua hasira katika kaunti, pendekezo la kujenga geti kwa Sh20 milioni liliibua msisimko pia kwenye mitandao ya kijamii.