Habari

Ghadhabu Pwani agizo la SGR likianza

August 6th, 2019 2 min read

Na MOHAMED AHMED

AGIZO la Serikali kuwa kuanzia Jumatano mizigo yote kutoka Bandari ya Mombasa iwe ikisafirishwa kwa reli ya SGR hadi Nairobi, limepokelewa kwa hasira na Wapwani.

Hapo Jumatatu wanasiasa na mashirika ya kijamii walitaja agizo hilo la Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru (KRA) na Mamlaka ya Bandari (KPA) kama unyanyasaji wenye nia ya kulemaza Wapwani kiuchumi.

Waliapa kupinga utekelezaji wa agizo hilo kupitia maandaano na bungeni, wakisema litasababisha kufungwa kwa biashara nyingi na maelfu ya wafanyikazi kufutwa.

Mkurugenzi mkuu wa Haki Africa, Hussein Khalid alisema uamuzi huo unaonyesha dhuluma ya wazi kwa Wapwani.

“Kama ni kuandamana basi tutaandamana. Hatuwezi kuruhusu Wapwani wabebe mzigo wa kulipa deni la SGR. Hii ni dhuluma ya wazi inayosononesha wakazi wa eneo hili,” akasema Bw Khalid.

Wenye malori ya uchukuzi wa mizigo, madereva na matani boi, wenye mabohari ya kuweka mizigo (CFS) na watoaji huduma zingine wanahofia kuporomoka kwa biashara zao.

Notisi ya KRA ilieleza kuwa mizigo yote ambayo inapaswa kwenda Nairobi pamoja na maeneo mengine mbali na Mombasa itachukuliwa katika Kituo cha Kontena cha Nairobi (ICD) baada ya kusafirishwa kwa SGR.

Hii imetokea wakati wakazi wa Pwani wameenda mahakamani kupinga hatua ya Serikali ya kupatia usimamizi wa bandari ya Mombasa kwa kampuni ya kibinafsi kutoka nje ya nchi ya Mediterranean Shipping Company.

Hapo jana, wabunge watatu kutoka Pwani walishutumu KRA kwa agizo la kusafirisha mizigo kwa SGR, wakiapa kuipinga Bungeni.

Wabunge hao Abulswamad Nassir (Mvita), Badi Twalib (Jomvu) na Khatib Mwashetani (Lunga Lunga) walisema watawasilisha hoja bungeni kutaka maelezo kuhusiana na uamuzi huo, ambao walisema utavuruga uchumi wa Pwani.

Bw Nassir alisema kuwa tayari amemwandikia barua Spika wa Bunge, Justin Muturi kuhusiana na suala hilo.

Katika taarifa ya pamoja na mashirika ya kijamii, viongozi hao walisema agizo hilo litapelekea kufa kwa biashara katika miji yote ya Pwani.

Bw Twalib alisema mamia ya vijana wataachwa bila kazi.

Naye Bw Mwashetani alisema agizo hilo linaondoa ushindani katika biashara za uchukuzi wa mizigo.