Michezo

Ghana ni watoto kwa Harambee Stars, asema Mwendwa

March 22nd, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

RAIS wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) Nick Mwendwa amesema Black Stars ya Ghana ‘haitoshi mboga’ kushinda Kombe la Bara Afrika (AFCON) litakalofanyika nchini Misri mwezi Juni 21 hadi Julai 19 mwaka 2019, tovuti ya GhanaWeb imemnukuu akiambia redio ya Angle FM mjini Kumasi.

“Hatutishwi na Black Stars. Mlikuwa timu kubwa sana miaka iliyoenda, lakini si wakati huu,” alisisitiza katika mahojiano na kituo hicho mnamo Alhamisi.

Kwa mujibu wa tovuti ya GhanaWeb, Mwendwa alichekelea Ghana kuwaita nyota Asamoah Gyan na Andre Ayew kama miamba katika kikosi hicho akisema, “wachezaji kama Gyan, Ayew; kivyangu, nadhani siku zao za kustaafu soka ya kimataifa zinapungua siku baada ya nyingine.”

Mwendwa ametoa maoni hayo saa chache baada ya Harambee Stars ya kocha Sebastien Migne kuondoka nchini Kenya mapema Alhamisi kuelekea Ghana kumenyana nao katika mechi ya mwisho ya Kundi F ya kufuzu kushiriki AFCON itakayoandaliwa uwanjani Accra mnamo Machi 23 saa tatu usiku.

Kenya na Ghana tayari zimeshafuzu kushiriki kipute hicho na zitakuwa zikikabana koo kuamua mshindi wa kundi hili. Kwa sasa, Kenya inaongoza kwa alama saba ikifuatiwa na Ghana (sita) nayo Ethiopia iko mkiani kwa alama moja. Ethiopia ilibanduliwa nje.

“Kwa hivyo, kama hamna wachezaji wapya, ambao tunafaa kuogopa, kama mntagemea hawa wawili kwenye AFCON, nawahurumia,” alisema na kuwataja Gyan na Ayew kama wanyonge.

Tovuti hiyo imenukuu Mwendwa akisema kwamba Ghana ilikuwa na kikosi thabiti mwaka 2010. “Nadhani mlikuwa na kikosi kizuri sana wakati wa Kombe la Dunia mwaka 2010 nchini Afrika Kusini na kwa sasa sijaona talanta mpya tangu wakati huo.”

Mabingwa mara nne Ghana wanalenga kumaliza ukame wa zaidi ya miaka 30 bila taji la Afrika. Nayo Kenya ilishiriki AFCON mara ya mwisho mwaka 2004.

Kikosi cha Kenya:

Makipa

Patrick Matasi (St Georges, Ethiopia), Farouk Shikalo (Bandari), John Oyemba (Kariobangi Sharks);

Mabeki

Erick “Marcelo” Ouma (Vasalund, Uswidi), Musa Mohammed (Nkana, Zambia), David Owino (Zesco, Zambia), Brian Mandela (Maritzburg, Afrika Kusini), Philemon Otieno (Gor Mahia), Benard Ochieng (Vihiga United), Joash Onyango (Gor Mahia);

Viungo

Erick Johanna (Brommapojkarna, Uswidi), Johanna Omollo (Cercle Brugge, Ubelgiji), Ismael Gonzales (Las Palmas B, Uhispania), Paul Were (Trikala, Ugiriki), Victor Wanyama (Tottenham Hotspur, Uingereza), Francis Kahata (Gor Mahia), Christopher Tangen Mbamba (Oskarshamns, Uswidi), Dennis Odhiambo (Sofapaka), Anthony Akumu (Zesco, Zambia);

Washambuliaji

Allan Wanga (Kakamega Homeboyz), Pistone Mutamba (Sofapaka), Masud Juma (Al Nassr, Libya).