Michezo

Ghana wajishaua taji la AFCON ni lao

April 15th, 2019 1 min read

NA CECIL ODONGO

RAIS wa Shirikisho la Soka la Ghana Dkt Kofi Amoah amejipiga kifua kwa kusema kwamba wakati umetimia kwa Black Stars kutwaa taji la Taifa Bingwa Barani Afrika(AFCON) mwaka huu wa 2019.

Akizungumzia droo ya makundi ya AFCON iliyoandaliwa Ijumaa Aprili 12 na kuiweka Ghana kwenye kundi F pamoja na Guinea-Bissau, Benin na Cameroon, Dkt Amoah alisema tayari wameshatwaa ubingwa huo hata kabla mtanange haujaanza.

“Kwangu hii droo tayari imetupatia ushindi wa moja kwa moja haswa kwa kuwa tutakumbana na wapinzani ambao mimi nawaheshimu ila katika fani ya soka, hawatuwezi,”

“Tunaenda kuchukulia kila mechi kwa uzito unaostahiki na kama taifa tuna historia pevu kwenye soka ambayo lazima tuilinde. Ingawa kila timu ilifuzu kwa kipute hiki kutokana na jasho lao, wakati umetimia kwa Ghana kutwaa taji hili baada ya kulikosa pembamba miaka ya nyuma,” akasema Dkt Amoah.

Black Stars itaanza kampeni ya AFCON 2019 itakayoandaliwa nchini Misri kwa kuvaana na Benin Juni 25 kisha ikabiliane na mabingwa wa zamani Cameroon Juni 26 kabla ya kuhitimisha mechi ya kundi Fdhidi ya Guinea-Bissau Julai 2.

Kabla ya kuelekea Misri, Black Stars inayojivunia wachezaji mahiri kama Andrew Ayew, Dede Ayew, Kwadwoh Asamoa, Asamoah Gyan kati ya wengine wanatarajiwa kushiriki mechi ya kujifua dhidi ya Nigeria ambao pia wanapigiwa upato kutamba kwenye kipute cha AFCON.