Gharama ya kustarehe yapanda – CBK

Gharama ya kustarehe yapanda – CBK

NA CHARLES WASONGA

WAKENYA waliathirika na mzigo mkubwa wa kupanda wa gharama ya kustarehe, michezo na masuala ya kitamaduni ndani ya kipindi cha zaidi ya miaka miwili, kufikia Juni 2022.

Hali hiyo ilipelekea wengi kupunguza kushiriki kwao katika baadhi ya shughuli hizo.

Gharama ya shughuli za starehe na burudani kama michezo ya mwasesere, michezo ya kuigiza, sinema, na ada za maeneo ya kujivinjari ilipanda kwa asilimia 3.06 mwezi Juni ilikilinganishwa na asilimia 0.74 wakati kama huo mwaka 2021.

Hii ni kulingana na data mpya ya hivi punde kutoka kwa Benki Kuu Nchini (CBK).

Ongezeko hili ni la juu zaidi kwa gharama ya shughuli za starehe na kujivinjari tangu Februari 2020 CBK ilipoanza kuchapisha data kwa misingi ya vipimo vinavyoangazia bei za huduma.

Shirika la Kitaifa la Takwimu (KNBS) liliangazia kwa kina vipimo hivyo na kubaini viwango vya mfumko wa bei.

KNBS inakadiria kuwa familia nchini hutumia karibu asilimia 1.7 za mapato yao kwa shughuli za starehe kila mwezi.

Kupanda kwa gharama ya shughuli hizo mwezi Juni, hata hivyo kulikuwa nyuma na kiwango cha kupanda kwa bei ya bidhaa na huduma za kimsingi, kama vile chakula na huduma kama maji, stima na uchukuzi.

Kwa kiwango kikubwa kupanda kwa gharama hiyo kulichangiwa na ongezeko la bei ya mafuta ambayo ilichangia kupanda kwa gharama ya kufanya biashara.

Mnamo Juni, mafuta aina ya dizeli iliuzwa kwa Sh140.91, petroli (Sh159.14) kwa lita moja, kiwango ambacho kinawakilisha ongezeko la kima cha asilimia 29.8 na asilimia 25 kwa bei ya bidhaa hizo mtawalia. Hii ni ikilinganishwa na mwaka wa 2021.

  • Tags

You can share this post!

Wakenya wavuma kwa wizi ng’ambo

Giroud akaribia rekodi ya mfungaji Thierry Henry nchini...

T L