Makala

Gharama ya lojing’i yasukuma makahaba kuchafua mazingira

March 5th, 2024 2 min read

NA MWANGI MUIRURI 

MFUMKO wa bei ya lojing’i Mjini Murang’a umelazimisha ‘wapenzi’ wa mahaba ya mkato kuzindua mbinu mpya kushiriki haja zao vichochoroni hasa nyakati za usiku.

Sawa na sekta zingine zinazoshuhudia kupanda kwa gharama, wamiliki wa vyumba hivyo vya kukodi kwa muda wameongeza bei jambo ambalo limeathiri wanaosaka burudani kupiga moyo pasi.

Hatua hiyo imewashinikiza kusaka ‘lojing’i’ mbadala – vichochoro, kilele chake kikiwa kuchafua mazingira.

Wakikwehepa mfumko huo wa bei, wanaacha nyuma uchafu hatari kwa afya na mazingira.

Kwa sasa, lojing’i Mjini Murang’a zimetinga kati ya Sh800 na Sh5, 500 (kulingana na hadhi ya uteja), huku wengi wa mahitaji ya mahaba ya mkato wakiwa ni mahasla wasio na hela.

Matokeo ya gharama hiyo ya juu ni vichochoro hivyo kugeuzwa kuwa kero ya kimazingira, washerati hao wakiacha mipira ya kondomu iliyotumika, vitambaa vya hedhi, walivyojipangusa navyo na pia shashi (tishue) zikiwa zimetapakaa kila mahali.

Kulingana na mwenyekiti wa muungano wa wanamazingira Murang’a Mashariki, Marvin Kigera, hali ni mbaya kiasi kwamba “nyuma ya uso wa Mji wa Murang’a ni ushahidi wa uozo wa kimaadili”.

Kigera anateta kwamba shirika lake limekuwa likilalamika kwa vitengo husika kama Idara ya Afya ya umma (PHO), Kamishna wa Kaunti na serikali ya Kaunti, kilio chao kikiangukia sikio lililowekwa pamba.

Alisema shida kuu ni kwamba wakishachafua vichochoro, nao walevi, chokoraa na watundu mtaani huchukulia maeneo hayo kama vyoo vya umma ambapo wao hujisaidia haja ndogo na kubwa huku wakazi wengine nao wakitupa taka za nyumbani kulikochafuliwa.

Alisikitikia wenye watoto akisema baadhi hucheza na mipira iliyotumika, wengine wakirukaruka juu ya kila aina ya uchafu kuweka jamii katika hatari ya mkurupuko wa maradhi.

Uchunguzi wa Taifa Leo Dijitali umebaini aibu za wazi Mjini Murang’a nyakati za usiku katika vichochoro hivyo, wapendanao wakiwa wameshikana na wengine wakijivinjari kwa kuvuta bangi.


Uchafuzi mazingira katika vichochoro vya Murang’a hushinikiza baadhi ya wakazi kuchoma taka zilizotapaka, hivyo basi kuchafua zaidi mazingira. PICHA|MWANGI MUIRURI 

Nyuma ya benki moja, tulikumbana na washirika wa mahaba wakitekeleza raha zao katika vichochoro.

Aidha, tulikutana na Bi Charity Kagendo, mkazi, ambaye mwendo wa saa 11 asubuhi alikuwa akichoma taka katika mojawapo ya vichochoro.

“Hawana hata aibu! Hushiriki ngono hadharani; nje yap loti ninayoishi,” Charity anasimulia.

Anasema si kisa kimoja, viwili au vitatu ameshuhudia na asubuhi kabla kusindikiza mwanawe aelekee shuleni hutangulia kwa kuchoma uchafu unaoachwa.

Aliteta hata hukutana na chupi zilizosahaulika maeneo hayo, walevi nao wakienda haja kiholela.

Waziri wa Mazingira katika Kaunti ya Murang’a, Bi Mary Magochi aliambia Taifa Leo Dijitali kwamba amepokea malalamishi hayo mara kadha.

“Nimekuwa nikipata malalamishi hayo na kisha nayapitishia vitengo husika. Ni suala la kufedhehesha kusikia kero hiyo haijakoma,” akasema afisa huyo, akiahidi kubadilisha mbinu inayotumika kuangazia suala hilo la aibu.

Bi Magochi aliwataka wenyeji wakikumbana na uchafu huo wawe wanaupiga picha na kumtumia, ili uwe ushahidi kuchukua hatua mahususi.

Waziri huyo aliteta kwamba hali ya wenyeji kuwasha moto hasa nyakati za usiku ili kujichomea taka ni kinyume na sheria, kwa kuwa ni hatari kwa mazingara na pia kwa binadamu.

Hata hivyo, aliahidi kwamba suluhu ya kidumu ipo njiani akisema serikali ya kaunti inashughulikia mikakati kukarabati vichochoro vya Mji wa Murang’a view salama.

“Kuna mpango wa vijana kushirikishwa katika ajira ya usafi mtaani na watatumwa katika vichochoro hivyo tata,” akasema.

Hali kadhalika, aliahidi kwamba askari wa halmashauri ya jiji watajukumika kushika doria kwenye vichochoro hivyo ili kutia nguvuni watundu wanaoharibu mazingira.

 

[email protected]