HabariSiasa

GHARAMA YA MAISHA: Kejeli na matusi kwenye akaunti za Rais mitandaoni

September 25th, 2018 2 min read

Na PETER MBURU

WAKENYA kwenye mitandao ya kijamii wameonekana kumvunjia Rais Uhuru Kenyatta heshima tangu alipotia sahihi Mswada wa Fedha 2018, huku kila chapisho kwenye akaunti za Rais ikipokelewa kwa cheche za matusi na kejeli za kila aina.

Tofauti na mbeleni ambapo machapisho ya Rais Kenyatta yangejibiwa kwa uchangamfu na Wakenya, ambao wengi ni vijana na watu waliosoma, kwa sasa Rais amekuwa akikejeliwa kila anapochapisha kuhusu shughuli za kitaifa anazofanya kwa wingi ambao sasa unahofisha.

Wakenya wengi wamekuwa wakimkemea kwa sababu alipitisha Mswada wa kuwapandishia ushuru kuwa sheria licha ya malalamiko yao, huku wengine wakimuonya kutokopa katika mataifa anayo zuru.

Jumatatu jioni, Rais Kenyatta alituma jumbe kadha kuhusu makongamano anayohudhuria nchini Marekani, lakini majibu aliyopata kutoka kwa Wakenya katika jumbe zote si ya kuridhisha.

“Mazungumzo ya umuhimu na chansela wa Australia H.E Sebastian Kurz na Rais wa Australia H.E Alexander Van der Bellen kuhusu kikao cha EU/Afrika kitakachofanyika Desemba na kongamano la Blue Economy litakalofanyika Novemba #UNGA,” Rais akatuma ujumbe huo kwenye akaunti zake za Facebook na Twitter.

Lakini bila kupoteza wakati, Wakenya walimvamia kwa kejeli na maneno yasiyo ya heshima, wingi wa waliomtumia jumbe chafu ukihofisha ikiwa Rias amepoteza heshima mbele ya anaowaongoza.

“Yani dunia haijatambua hapa kuna mtu anayezunguka akila chakula chao na kukopa pesa zao tu?”akauliza Justus Too.

“Umuhimu gani, muulize chansela wa Australia ikiwa Waaustralia wenzake wanalala njaa, muulize kama ufisadi ni kivutio cha utalii kama Kenya,” Guanta Namo akajibu.

Jeremy Wakamu naye alishangaa “Unatarajia vipi nijalishwe nawe kukutana sijui na nani wa kutoka wapi wakati watu wetu kijijini wanalipa pesa nyingi zaidi kununua mafuta ya taa ili waangaze nyumba, pesa zinazotoshana na zinazotumia lori za brookside kwa dizeli ambazo huwabebea maziwa  na kuwalipa vibaya.”

“Fanya chochote unachoweza huko, lakini tafadhali usirudi na deni jingine,” akasema Jacob Man Untd.

Nick Tuwei alimwambia Rais “Hatutasahau! Hautatufunika! Hautatuziba macho! Kutana na yeyote unayetaka, sema chochote kizuri kuwahusu. Hata waambie wakupe ugeni huko. Ukiwa mbali tunahisi kupungukiwa na mzigo wa ushuru ulioacha. Ombi langu ni ukiamua kurudi, tafadhali usije na madeni zaidi. Ni hayo tu kwa sasa.”

Rais aidha alituma ujumbe kuhusu kongamano jingine akisema “Nilihudhuria kongamano la kuhamasisha kuhusu hatua dhidi ya dawa za kulevya kuchukuliwa lililoongozwa na Rais wa US Donald Trump, kando na lile la 73 la UN #UNGA.”

Lakini Wakenya hawakumpa nafasi kupumua.

“Mara ya mwisho niliwacha umepunguza matumizi ya ziara za serikali na mashirika mengine ukisema ni kwa sababu ya matumizi mazuri ya ushuru, iweje ulisafiri?” akauliza Lawre Hernandez Koome.

Hon Paul Ochoke Ogwankwa alisema “Mjulishe Trump kuwa Kenya sasa inauza mafuta taa kwa Sh120kwa lita na kuwa tunahudumu kwa sare za China.”