Kimataifa

GHARAMA YA MAISHA: Mkate wa Sh1,500

May 31st, 2018 1 min read

Na VALENTINE OBARA

UKITAKA kufurahia mkate wako wa kila siku, itakubidi kutumia Sh1,580 kununua kilo moja ya boflo ukiwa jijini Seoul, Korea Kusini.

Ingawa Wakenya hulalamikia gharama ya juu ya maisha, mkate wa kilo moja humu nchini huuzwa kwa Sh125.

Haya ni kwa mujibu wa ripoti ya utafiti kuhusu majiji ambapo hali ya maisha ni ghali zaidi ulimwenguni, uliofanywa na shirika la Economist Intelligence Unit lililo Uingereza.

Kulingana na ripoti hiyo, jiji la Singapore ndilo ghali zaidi kuishi ulimwenguni, likifuatwa na Paris (Ufaransa), Switzerland (Zurich) na Hong Kong (Uchina).

Ilibainika kuwa katika majiji hayo, gharama ya maisha iko juu mno hasa kwa ununuzi wa bidhaa za matumizi nyumbani, mavazi na kodi ya nyumba. Hata hivyo itakumbukwa kuwa majiji hayo yako katika nchi ambazo zimeendelea kiuchumi.

Majiji ambayo yalipatikana kuwa na gharama ya chini zaidi ya maisha yako katika mataifa ambayo yanakumbwa na changamoto mbalimbali kama vile kivita na uongozi mbaya.

“Kwa kueleza kirahisi, majiji ya gharama ya chini pia huwa na hali inayofanya iwe vigumu kuishi huko,” ripoti hiyo inasema.

Gharama ya chini zaidi ya maisha ilipatikana Damascus (Syria), Caracas (Venezuela), Almaty (Kazakhstan), Lagos (Nigeria) na Bangalore (India).

Katika jiji la Damascus, boflo ya kilo moja ya mkate hugharimu dola 0.60 (Sh60), kwa mujibu wa ripoti hiyo.