Kimataifa

Ghasia baada ya mahakama kuamuru wanawake waruhusiwe hekaluni

October 23rd, 2018 2 min read

BBC na PETER MBURU

KERALA, INDIA

KULIKUWA na maandamano na fujo katika hekalu moja nchini India, baada ya Mahakama Kuu ya nchi hiyo kutoa uamuzi wa kutatanisha, ilipoamua kuwa wanawake wanapasa kuabudu humo, jambo ambalo halijawahi kuonekana.

Hekalu hilo la Sabarimala lililopo katika mji wa Kerala kusini mwa India limekuwa na imani ya aina yake kuwa ni wanaume tu wanaoshiriki, lakini wiki hii mahakama ikaamua kuwa hata wanawake wanapaswa kushiriki ibada.

Uamuzi huo wa korti ulisababisha maandamano makubwa ya fujo, huku zaidi ya polisi 100 wakitumwa kutuliza hali wakati wanawake wawili ambao walijaribu kuingia hekalu hilo kwa mara ya kwanza wakitupiwa mawe na waandamanaji wenye ghadhabu walioziba njia.

Polisi zaidi ya 100 waliwalinda, mwandishi Kavitha Jagdal na mwanaharakati wa masuala ya kijamii, Rehana Fathima kuzuia mawe waliyokua wanatupiwa na waandamanaji walipokuwa wakitembea kilomita tano sawa na maili tatu kuelekea kwenye hekalu hilo.

Lakini iliwalazimu kurudi baada ya kusimamishwa na wafuasi wa hekalu hilo mita chache kutoka kwenye hekalu hilo.

Waandamanaji pia wamejumuisha wanawake wengi ambao wameshiriki katika migomo, kuziba barabara na kukagua magari yanayokwenda hekaluni yakiwa yamebeba mwanamke yeyote aliye kati ya umri wa miaka 10 mpaka 50.

Hekalu hilo linavutia mamilioni ya wafuasi huko India, huku baadhi ya wanawake wakichukulia hali ya kunyimwa kuingia hekaluni kuwa upendeleo.

Waandamanaji hao sasa wamepinga amri za korti wakisema zinaenda kinyume na matakwa ya Mungu, akiitwa Ayappa.

Waumini wa dini ya Kihindu wanawachukulia wanawake wanaopata hedhi kutowa watakatifu na hivyo huwazuia kushiriki shughuli za kidini.

Hekalu la Sabarimala ni moja kati ya mahekalu machache ambayo huwazuia kabisa wanawake walio katika umri wa kupata hedhi kuingia hekaluni.

Lakini wafuasi wa dini hiyo wamejitetea kuwa kuwakataza wanawake kuingia katika hekalu hilo si kwa sababu ya hedhi pekee, ila pia kwa sababu ya kutii matakwa ya Mungu wao ambaye waaamini ni taratibu zake ili awabariki.

Kila mwaka mamilioni ya wafuasi wa kiume wa dini hiyo hupanda mlima bila viatu ili kuliona kaburi, mbali na kufunga kwa siku 41 na kuepuka kuvuta sigara, pombe, nyama, ngono au kuwasiliana na wanawake walio katika hedhi kabla ya kuanza safari.

Kila mungu katika imani ya Kihindu ana haiba yake na upekee wa visa vyake mwenyewe, na mungu Ayappa hana tofauti.

Mungu Ayyappa hana mahusiano kwani amechukua kiapo cha useja, yaani kutoishi na mwanamke.

Kwa mujibu wa hadithi, Ayappa alizaliwa baada ya muungano kati ya miungu wawili wa kiume ambao wamempa nguvu na uwezo wa kumshinda pepo wakike ambaye alikuwa akisumbua hadi wakati huo.