Kimataifa

Ghasia zachacha Hong Kong ikipinga utawala wa China

November 4th, 2019 2 min read

NA AFP

GHASIA zinaendelea kushuhudiwa mjini Hong Kong baada ya raia kupinga vikali udhibiti wa eneo hilo na serikali kuu ya China yenye makao yake jijini Beijing.

Hapo jana, polisi walilazimika kufyatua risasi na vitoa machozi hewani maelfu ya raia wakiandamana kupinga sera za China kutumika kwenye uongozi wa jiji hilo linalojitawala kivyake.

Waandamanaji hao walipiga mawe vituo vya kibiashara vinavyoaminika kumilikiwa na wafanyabiashara wanaounga serikali ya China ikiwemo afisi ya Shirika la habari la Xinhua.

Polisi nao waliwakabili waandamanaji hao walijitahidi sana kukabiliana na waandamanaji huku taarifa zikisema zaidi ya waandamanaji 100 walikamatwa na kuwekwa ndani ya magari matatu ya polisi hadi maeneo yasiyojulikana.

Kupitia taarifa, Xinhua ilikashifu waandamanaji walioshambulia afisi zake na kuwataja kama watu wasiofahamu wanachokitenda.

Maandamano hayo yanakuja baada ya serikali ya China mnamo Ijumaa kusema kwamba haitavumilia mabadiliko yoyote kwenye utawala wa serikali ya Hong Kong na nia ya uongozi huo kuanzisha masomo yanayowasisitizia raia wao kuonyesha uzalendo kwa taifa lao.

Huku waandamanaji jijini Hong Kong wakiwa hawaonyeshi dalili zozote za kukata tamaa na kuwa watulivu, utawala wa Beijing nao umekataa kuridhia mapendekezo ya kuwapa waandamanaji hao uhuru na demokrasia wanayopigania.

“Serikali yote ya Hong Kong inadhibitiwa na utawala wa China na sasa lazima tujitokeze na tupiganie demokrasia na haki yetu. Hatutakata tamaa hadi tupate kile tunachohitaji,” akasema Gordon Tsoi, 18 ambaye ni kati ya waaandamanaji wanaopigania utawala huru wa mji huo.

Polisi ambao wamelaumiwa pakubwa kwa kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya raia wamekuwa wakikataa kuidhinisha notisi ya kuruhusu maandamano ya amani yaandaliwe japo mara nyingi raia huwapuuza.

Baada ya miezi kadhaa ya maandamano, makabiliano kati ya polisi na raia yamekuwa jambo la kawaida huku Umoja wa Kimataifa(UN) ukionya kwamba hali isipodhibitiwa, uhasama kati ya China na raia wa Hong Kong utasambaratisha ukuaji wa mji huo kabisa.

“Uhuru wa kujikusanya au kuandaa mkutano unazidi kukandamizwa kwa kuwa polisi wapo kila mahali. Hata hivyo, tutazidi kupigania haki zetu za kikatiba,” akaandika mmoja wa waandamanaji Joshua Yong kupitia Twitter.

Tangu aingie mamlakani, Rais Xi Jinping amekuwa akilaumiwa kwa kukandamiza uhuru wa raia wa Hong Kong.