Michezo

Ghost Mulee kusaidiwa na Musa Otieno, William Muluya kuinoa Harambee Stars

October 21st, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

LICHA ya kuagana rasmi na Harambee Stars miaka 10 iliyopita, kocha veterani Jacob ‘Ghost’ Mulee yuko pazuri zaidi kupokezwa mikoba ya timu ya taifa ambayo mkufunzi Francis Kimanzi alipokonywa na Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) mnamo Oktoba 20, 2020.

Mulee, 52, kwa sasa ni mtangazaji wa kituo cha Radio Jambo, mchanganuzi wa masuala ya soka na kocha wa akademia ya kandanda anayoimiliki jijini Nairobi. Mbali na kumpokeza fowadi Michael Olunga malezi ya kusakata kabumbu, Mulee anakumbukwa zaidi kwa mafanikio ya kuongoza Stars kutinga fainali za Kombe la Afrika (AFCON) zilizoandaliwa nchini Tunisia mnamo 2004.

Kwa pamoja na wenzake Zedekiah ‘Zico’ Otieno (kocha msaidizi) na Lawrence Webo (kocha wa makipa) kwenye benchi ya kiufundi, Kimanzi aliagana rasmi na Stars mnamo Jumanne. Chini ya ukufunzi wake, Stars walipoteza mechi mbili pekee kati ya 10 alizozisimamia kwa kipindi cha miezi 14.

Kimanzi ambaye pia amewahi kuwanoa Tusker FC na Mathare United, aliaminiwa kuwa mrithi wa Mfaransa Sebastien Migne mnamo Agosti 2019, mwezi mmoja baada ya fainali za AFCON nchini Misri. Hadi kuteuliwa kwake kwa mara ya tatu, aliwahi kudhibiti mikoba ya Stars kwa vipindi viwili tofauti kati ya Novemba 2008 na Januari 2009 kisha Novemba 2011 hadi Juni 2012.

Mbali na Mulee ambaye pia amewahi kuhudumu kambini mwa Stars katika vipindi vinne tofauti, wakufunzi wengine wanaohusishwa na mikoba ya timu ya taifa ni Francis Baraza wa Biashara United nchini Tanzania na Twahiri Muhiddin ambaye ni sasa ni mkurugenzi wa kiufundi kambini mwa Bandari FC.

Mwingine ni nahodha wa zamani wa Stars, Musa Otero Otieno ambaye aliwahi kuwa kocha msaidizi wa timu ya taifa. Kwa mujibu wa mdokezi wetu kutoka Kandanda House ambayo ni makao makuu ya FKF, Otero na William Muluya wa klabu ya Kariobangi Sharks wanapigiwa upatu kuwa msaidizi wa Mulee.

Mulee alijitosa rasmi kwenye ulingo wa ukufunzi ndani ya kikosi cha Stars mnamo 2003 na akaongoza kikosi hicho kunogesha fainali za AFCON mwaka mmoja baadaye. Aliagana na Stars mwishoni mwa 2004 kabla ya kurejeshewa mikoba kwa mara nyingine mnamo 2005, 2007 na Disemba 2010 alipoongoza timu ya taifa kushiriki fainali za Cecafa Senior Challenge zilizoandaliwa jijini Dar es Salaam, Tanzania.

“FKF imefikia maamuzi ya kumteua Mulee kuwa kocha mpya wa Stars. Anajivunia tajriba pevu na uzoefu mkubwa ambao utawezesha Stars kufuzu kwa fainali zijazo za AFCON 2021 nchini Cameroon na Kombe la Dunia mnamo 2022 nchini Qatar,” akasema mdokezi wetu kwa kusisitiza kwamba Mulee atapokezwa mkataba wiki hii.

Kibarua cha kwanza cha Mulee kambini mwa Stars ni kuongoza kikosi hicho kuvaana na Comoros kwenye michuano miwili ijayo ya kufuzu kwa fainali za AFCON 2021. Kenya imetiwa kwenye Kundi B kwa pamoja na Comoros, Togo na mabingwa mara saba, Misri.

Chini ya Kimanzi, Stars walianza kampeni zao za kufuzu kwa fainali hizo dhidi ya Misri kwa sare ya 1-1 mnamo Novemba 14, 2019 ugenini kabla ya kusajili matokeo sawa na hayo dhidi ya Togo mnamo Novemba 18, 2019 jijini Nairobi.

Kocha huyo pia aliongoza Stars kuzamisha Zambia, baada ya kubwaga Zanzibar, Sudan na Tanzania mara mbili. Alisaidia Kenya kusajili sare dhidi ya Uganda kirafiki kabla ya kikosi chake kuzidiwa maarifa na Eritrea na Msumbiji.