MakalaSiasa

Gichuhi atafaulu kumaliza migawanyiko katika LSK?

February 26th, 2018 3 min read

Mwenyekiti mpya wa Chama cha Wanasheria nchini (LSK), Bw Allen Gichuhi. Picha/ Maktaba

Na BENSON MATHEKA

UCHAGUZI wa  maafisa wa Chama cha Wanasheria nchini (LSK), ulikiacha kikiwa kimegawanyika zaidi kwa misingi ya kisiasa nchini na kuzua wasiwasi ikiwa uongozi mpya utatekeleza majukumu yake ya kuikosoa serikali ipasavyo.

Mwenyekiti mpya wa chama hicho, Bw Allen Gichuhi, anakabiliwa na kibarua kigumu kuunganisha chama hicho ambacho wanachama wamegawanyika katika mirengo ya kisiasa ya Jubilee na NASA na kwa misingi ya umri.

Japo wadadisi wamemtaja Gichuhi kuwa mwanamageuzi, kuna wale wanaoamini kwamba Bw Gichuhi anaegemea upande wa chama cha Jubilee na LSK itakosa makali ya kuikosoa serikali.

Wanasema kwamba msimamo wa Bw Gichuhi ni tofauti na wa mtangulizi wake Isaac Okero ambaye serikali iliamini aliegemea upande wa upinzani. “Uongozi mpya wa LSK ni tofauti na uliotangulia.

Mwenyekiti Allen Gichuhi anaaminika kuwa na msimamo wa kadiri. Kuna wale wanaoamini kwamba alikuwa kibaraka cha serikali kumzima mpinzani wake James Mwamu anayejulikana kwa kuwa na msimamo huru,” asema mwanasheria mmoja ambaye aliomba tusitaje jina kwa sababu ni mwanachama wa baraza jipya la LSK.

 

Kuzimwa kwa Havi

Kulingana na wakili huyo, kuzimwa kwa wakili Nelson Havi aliyeongoza mawakili vijana ambao ndio wengi katika chama hicho, kulimpa Bw Gichuhi nafasi ya kushinda.

Mahakama ya rufaa ilikataa kusimamisha uchaguzi huo kufuatia ombi la  Bw Havi ambaye amekuwa mstari wa mbele kutetea muungano wa NASA.

Bw Havi alitaka uchaguzi huo usimamishwe baada ya maafisa wa LSK kumzuia kugombea kiti cha uenyekiti kwa sababu ya kutotimiza kigezo cha miaka 15 akihudumu kama wakili.

Akiongea baada ya kushinda kiti hicho, Bw Gichuhi aliweka wazi kuwa uongozi wake hautakuwa wa kukabili serikali ila wa kushauriana nayo, jambo ambalo wadadisi wanasema itakuwa ni kuua jukumu la LSK.

“Hiki ni chama kilicho na jukumu pana la kupiga serikali darubini. Huwezi ukashauriana na serikali inayokandamiza wananchi wa kawaida. Ni lazima LSK ichukue msimamo thabiti kuhusu masuala yanayoikabili nchi.

Msimamo huo mara nyingi huwa wa kuhakikisha serikali imewajibika na si kuidhinisha maamuzi yake,” asema wakili mwingine ambaye pia ni mwanachama wa baraza la LSK.

 

Mwanamwageuzi

Bw Gichuhi alisema si lazima LSK itumie makabiliano ili kuikosoa serikali, kauli ambayo wakili Profesa George Wajackoyah anakubaliana nayo. “Ninamjua Bw Gichuhi kama mwanamageuzi.

Ni mtu anayependa kushauriana kwa upana na atabadilisha LSK,” asema Bw Wajackoyah. Bw Gichuhi mwenyewe alionekana kuelewa kwamba chama kimekumbwa na migawanyiko.

“Ajenda yangu ya kwanza itakuwa ni kuunganisha wanachama wa LSK  ili tuweze kufanya kazi pamoja. Tunataka kurudisha chama katika hali yake ya awali,” alisema Bw Gichuhi ambaye katika kampeni zake wengi waliamini alikuwa mradi wa serikali.

“Ninajua kwamba ninachukuliwa kuwa  kibaraka wa Jubilee na wengine wananihukumu kwa misingi ya kikabila. Hao ni watu ambao hawanielewi. LSK haifai kuunga mirengo ya kisiasa. Siungi mrengo wowote wa kisiasa,” alisema Bw Gichuhi ambaye ni mtaalamu wa sheria za usimamizi mwenye tajriba pana.

Katika kampeni, baadhi ya mawakili walidai kwamba Bw Gichuhi alifadhiliwa na serikali ilhali Nelson Havi alikuwa akifadhiliwa na NASA.

Kinachowafanya mawakili wengi ambao walisusia uchaguzi huo kuamini kwamba Gichuhi anaegemea  upande wa serikali ni jinsi  wanasiasa wa Jubilee walivyomtetea wakiongozwa na kiongozi wa wengi katika seneti Kipchuma Murkomen ambaye pia ni wakili.

Bw Murkomen alikuwa miongoni mwa wanasiasa wa kwanza kumpongeza Bw Gichuhi baada ya kushinda.

 

Hatari

“Japo anaweza kujiwakilisha kama mwanamageuzi na baadhi yetu tunamjua hivyo, kuhusishwa kwake na Jubilee kunaweka chama katika hatari ya kutotekeleza majukumu yake ya kukosoa serikali,” asema wakili mmoja ambaye amekuwa karibu na Bw Gichuhi kwa miaka mingi.

Wakili huyo anakiri kwamba iwapo Bw James Aggrey Mwamu angeshinda uchaguzi huo, LSK ingepata mwamko mpya kwa sababu ya ufahamu wake wa masuala ya kisheria na ujasiri wake wa siasa za Kenya na ukanda wa Afrika Mashariki kwa jumla.

Bw Gichuhi alipata kura 2,675 naye Mwamu akapata 2,145  katika uchaguzi uliosimamiwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Katika kile kinachoonwa kama sura  mpya katika LSK, naibu wa Gichuhi ni Harriette Chiggai ambaye aliapa kuungana na mwenyekiti wake kubadilisha LSK bila makabiliano.

Wanachama wa baraza la LSK ni Bi Roseline Odede Maria Mbeneka, Eric Wafula, Aluso Ingati, Boniface Akusala, Bernard Ng’etich, Jane Masai, David Njuguna, Hetrine Kabita, Caroline Kamende na Ndinda Kinyili.

Bw Havi ambaye aliongoza mawakili vijana, ambao awali walitishia kususia uchaguzi, alimuunga Bw Mwamu uamuzi ambao ulizua vita mtandaoni kati yake na Bw Murkomen.