Habari

Gideon ahimizwa aanzishe ushirika na jamii ya Luhya

February 15th, 2020 2 min read

SHABAN MAKOKHA na CHARLES WASONGA

BAADHI ya wabunge kutoka jamii ya Abaluhya, sasa wanamtaka Seneta wa Baringo Gideon Moi kubuni muungano wa kisiasa na jamii hiyo kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.

Wabunge wa chama cha ANC, Ayub Savula (Lugari) na Tindi Mwale (Butere), wamemtaka Seneta Moi ambaye alikabidhiwa uongozi wa kisiasa wa familia ya Rais wa zamani Daniel Moi aliyezikwa Jumatano, kushirikiana na mgombea urais kutoka jamii ya ‘Mulembe‘.

“Tunataka Gideon abuni muungano na mgombeaji urais ambaye sisi kama jamii ya Mulembe‘ tutamteua. Mzee Moi alipenda zaidi watu wetu na hakutubagua wakati wa utawala wake,” akasema Bw Savula akiongeza kuwa muungano kama huo utawezesha eneo la magharibi kupata angalau nyadhifa nane za uwaziri katika serikali ijayo.

Naye Bw Mwale akasema: “Tunatambua hadhi ambayo Gideon alipewa na familia yake. Kwa hivyo tunamuomba afanye kazi nasi alivyofanya marehemu babake. Tunataka kubuni muungano naye kuelekea uchaguzi mkuu ujao.”

Seneta Moi alipewa rungu ya usemi wa kisiasa na ndugu yake mkubwa Raymond Moi wakati wa mazishi ya baba yao kule Kabarak, Nakuru.

Hatua ya Gideon kupokezwa rungu imeibua maswali kuhusu endapo atachukua nafasi ya Mzee Moi ya kuwa kigogo wa kisiasa katika eneo zima la Rift Valley.

Marehemu alisalia kuwa kiongozi wa kisiasa wa eneo hilo hata baada ya kustaafu na kumpokeza Mwai Kibaki uongozi wa nchi mnamo mwaka wa 2002.

Hii ndiyo maana viongozi wengi wamekuwa wakizuru Kabarak kusaka ushauri wa kisiasa kutoka kwa Mzee Moi.

Bw Savula ambaye pia ni naibu kiongozi wa ANC alisema Seneta Moi anafaa kutambuliwa kama msemaji rasmi wa jamii ya Wakalenjin kwa “sababu ana uwezo wa kuongoza eneo zima la Rift Valley.”

Mbunge huyo wa Lugari alimwalika Seneta Moi kuzuru eneo la Magharibi ili kujitafutia uungwaji mkono kisiasa.

Bw Savula alisema hayo alipohudhuria mkutano wa wajumbe wa ANC mjini Butere kupanga mikakati ya kampeni za chama hicho kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.

Bw Mwale alisema muungano kati ya mgombeaji urais kutoka jamii ya Abaluhya na Seneta Moi utaibuka na ushindi katika uchaguzi mkuu wa 2022.

“Tunamtaka Gideon kuongea na viongozi wakuu wa kisiasa kutoka jamii yetu kama vile Kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi, Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya na kiongozi wa Ford Kenya Moses Wetang’ula ili tubuni muungano wenye nguvu kuelekea 2022,” akasema Mwale.

Kauli za wabunge hao zinajiri siku chache baada ya Bw Mudavadi kuwapuuzilia mbali wanasiasa wa mrengo wa ‘Tangatanga’ ambao wamekuwa wakimshinikiza kubuni muungano na Naibu Rais William Ruto kueleleza uchaguzi mkuu ujao.

Kiongozi huyo wa ANC alisema kuwa chama chake kitafanya uamuzi kuhusu suala hilo wakati “unaofaa” lakini sio kutokana na shinikizo kutoka kwa wanasiasa.