Habari MsetoSiasa

Gideon arithi rungu la Mzee

February 12th, 2020 1 min read

Na JUMA NAMLOLA

MTOTO mkubwa wa Mzee Moi, Raymond alimpokeza rasmi mdogo wake fimbo ya baba yao.

Mbunge huyo wa Rongai, alimkabidhi Seneta Gideon (Baringo), ‘fimbo ya Nyayo’ iliyobebwa na marehemu Mzee Moi kwa miaka 24 ya utawala wake.

Ingawa haijulikani kama ni fimbo ile ile, hatua hiyo inaonekana kuwa ishara ya kumpandisha seneta Moi ngazi kisiasa.

“Najua mimi ndiye mkubwa katika familia, lakini si mkubwa kisiasa. Ndugu yangu Gideon ndiye anayestahili kurithi fimbo hii yam zee,” akasema Bw Raymond, mwishoni mwa hotuba za waombolezaji katika Chuo Kikuu cha Kabarak, Nakuru.

Seneta Moi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kitaifa wa chama cha KANU, alipokea fimbo hiyo na kuahidi kusema mengi baada ya msiba.

Hatua hiyo huenda ikawa gumzo katika siku kadhaa zijazo, ikizingatiwa kuwa chama hicho tayari kimetangaza mipango ya kujifufua.

Aidha, huenda ikaendeleza ubabe wa kisiasa kati ya Bw Gideon na Naibu Rais William Ruto kuhusu msemaji wa Binde La Ufa.