HabariSiasa

Gideon aweka mikakati kuteka nyoyo za vijana

August 5th, 2020 2 min read

Na FRANCIS MUREITHI

SENETA wa Baringo Gideon Moi amebuni mbinu mpya ya kujivumisha kuwa Rais mnamo 2022, na wakati huo huo kuyeyusha umaarufu wa Naibu Rais Dkt William Ruto katika eneo la Bonde la Ufa na maeneo mengine nchini.

Ameunda Baraza la usimamizi wa vijana kwenye chama chake cha Kanu ambalo linaongozwa na Seneta wa Pokot Magharibi Samuel Poghisio, Cornelius Kipchumba na Mary Anne Njambi aliyewania kiti cha eneobunge la Molo katika uchaguzi mkuu wa 2017.

Mwenyekiti wa kitaifa wa vuguvugu la wanawake wa Kanu Elizabeth Kimkung pia yupo kwenye baraza hilo.

Mbinu ya Bw Moi ya kuwakumbatia vijana inatumiwa wakati ambapo Dkt Ruto amekuwa akijivumisha kote nchini kupitia viongozi vijana.

Dkt Ruto tayari anatumia vijana kupenyeza kisiasa maeneo ya Nyanza na Mlima Kenya ili kujiweka pazuri kushinda Urais mnamo 2022.

Kwa kuwa Dkt Ruto amekuwa akikutana na ujumbe wa viongozi nyumbani kwake Karen na Sugoi, Bw Moi naye ameanza kuwapokea viongozi nyumbani kwa babake, marehemu Rais Mstaafu Daniel Arap Moi, Kabarak, katika Kaunti ya Nakuru.

Seneta wa Kajiado Philip Mpaayei aliongoza ujumbe wa vijana kumtembelea Bw Moi wikendi iliyopita.“Maandishi yapo wazi ukutani kwa kila mwenye macho kuyaona. Hauhitaji uambiwe ndio uyaone,” akasema Bw Mpaayei akizungumzia siasa za urithi.

Kulingana na waliohudhuria mkutano huo, Seneta Mpaayei na vijana kutoka Kajiado waliahidi kumuunga mkono Bw Moi kwenye kura ya 2022.Wandani wa Bw Moi nao wanasema mbinu hiyo mpya ya kukutana na vijana itaendelea huku wengine wengi wakialikwa wafike Kabarak hivi karibuni.

Hatua ya Bw Moi kukutana na vijana huku akijiimarisha kuwania uongozi wa nchi kwa mara ya kwanza mnamo 2022, inatokana na kile wandani wake wanasema ni kupanda kwa umaarufu wa Dkt Ruto miongoni mwa vijana nchini.

Hata hivyo, mmoja wa viongozi vijana kwenye mrengo wa Dkt Ruto Joseph Kibusia amesema mbinu hiyo haitamnufaisha Bw Moi kwa kuwa ameianzisha akiwa amechelewa na vijana wengi tayari wako kwa Dkt Ruto.

“Iwapo Gideon ataidhinishwa na Rais Uhuru Kenyatta au la, Dkt Ruto tayari yupo kifua mbele. Hawezi kufikia umaarufu wa Naibu Rais unaoenezwa nyanjani na vijana wengi wa makabila mbalimbali kote nchini,” akasema Bw Kibusia.

Kimani wa Kimani ambaye ni Katibu mtendaji wa Kanu mjini Nakuru hata hivyo alisema vijana hukimbilia tu kwa Dkt Ruto kupokea fedha na hawatamuunga mkono 2022.“Vijana wanaofurika kwa Ruto wana njaa na hukimbilia fedha zake.

Hata hivyo, sisi tunaounga mkono Gideon huwasaidia vijana kushiriki miradi ya kuwainua kiuchumi kama ufugaji wa kuku, ng’ombe na miradi ya kuchimba visima,” akasema Bw Kimani.

Mwanasiasa mkongwe na Waziri wa zamani Musa Sirma alisifu Bw Moi kwa mbinu yake mpya na akamshauri ashirikiane na viongozi wote nchini.

“Wale wanaomuunga mkono Naibu Rais wanajua haja yao ni pesa lakini sisi tuko nyuma ya Gideon ili taifa liwe bora na watoto wetu wahakikishiwe maisha mazuri. Hiyo ndiyo maana naunga mkono mbinu yake ya kukutana na vijana kujenga himaya yake kisiasa,” akasema mbunge huyo wa zamani wa Eldama Ravine.