Gikaria, Arama, Ngunjiri wahojiwa kuhusu genge la ‘Confirm’ Nakuru

Gikaria, Arama, Ngunjiri wahojiwa kuhusu genge la ‘Confirm’ Nakuru

JOSEPH OPENDA NA MERCY KOSKEI

WABUNGE watatu kutoka Nakuru wanachunguzwa kuhusiana na madai ya kufadhili genge hatari la ‘Confirm’ linaloshukiwa kutekeleza mauaji jijini Nakuru na viungani mwake.

Mbunge wa Nakuru Mjini Mashariki David Gikaria, Samuel Arama (Nakuru Mjini Magharibi) na Kimani Ngunjiri wa Bahati, Jumatatu waliandikisha taarifa kwa polisi kuhusu shughuli za genge hilo.

Mtu mwingine anayechunguzwa ni mwanawe Bw Gikaria ambaye maafisa wa usalama wanaamini amekuwa akiunga mkono shughuli za wahalifu hao.

Mshirikishi wa Bonde la Ufa Maalim Mohamed amethibitisha kuwa wabunge hao watatu walihojiwa katika afisi za Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) jijini Nakuru kuhusu suala hilo.

Bw Maalim alisema Bw Ngunjiri alifaa kutoa maelezo zaidi kuhusu shughuli kuhusu genge hilo baada ya kutoa madai kuwa kundi la vijana lilisafirishwa kutoka Nairobi kuwahangaisha watu wa Nakuru msimu huu wa uchaguzi.

Afisa huyo wa utawala vile vile alieleza kuwa mbunge huyo alijiwasilisha kwa afisi ya Kamishna wa Kaunti ya Nakuru akidai kuwa na habari kuhusu magenge ya fulani ya wahalifu katika kaunti ya Nakuru.

“Anafaa kuelezea zaidi kuhusu magenge ambayo alikuwa akirejelea. Hatusemi kuwa ni washukiwa, lakini tumtaka Bw Ngunjiri na wenzake kutoa habari zitakazosaidia katika uchanguzi,” akasema Bw Maalim.

Hata hivyo, aliongeza kuwa Bw Arama, Bw Gikaria na mwanawe, wamekabiliwa na tuhuma za kufadhili na kutoa ulinzi kwa magenge fulani ya wahalifu.

Duru za polisi pia zimefichua kuwa wabunge hao wamekuwa wakiwalipia faini wanachama wa genge la “Confirm” wanapokamatwa.

Mbw Arama na Gikaria walifika katika afisi za DCI Jumatatu asubuhi na wakahojiwa kwa saa kadha kabla ya kuachiliwa.

Hata hivyo, baada ya kuondoka, Bw Arama alikana madai kuwa alihojiwa na maafisa wa DCI, akisema alifika katika afisi hizo kwa shughuli tofauti.

Alikana kuwa na uhusiano na genge lolote la wahalifu akishikilia kuwa genge la “confirm” haliendeshi shughuli zake katika eneo bunge lake.

“Nilifika hapa kujadili masuala mengi na ndiposa nikagundua kuwa Bw Gikaria pia alikuwepo hapa. Hakuna jambo lenye uzito kwa sababu tulikuwa tukipanga masuala mengine yanayoathiri kaunti,” akasema Bw Arama.

Bw Mohamed alifichua kuwa polisi wamewakamata watu 128 wanaoshukiwa kuwa wanachama wa genge la ‘confirm’ katika operesheni inayoendelea dhidi ya magenge haramu katika eneo hilo.

Hata yanajiri baada ya Waziri wa Usalama Fred Matiang’i kuamuru kutumwa kwa kikosi maalum Nakuru kupambana na genge hilo.

Genge la confirm na makundi mengine, yamehusishwa na visa vya wizi, ubakaji na msururu wa mauaji ya kikatili katika eneo Mawanga, kaunti ndogo la Bahati.

Ingawa polisi wangali wanachunguza mauaji hayo, ripoti za ujasusi zinasema kuwa huenda wanachama wa genge hilo ndio walihusika na mauaji hayo.

Katika muda wa wiki mbili wanawake wameuawa katika eneo la Mawanga, na maeneo ya karibu, katika hali ya kutatanisha.

Wakazi sasa wanaishi kwa hofu huku wengine wakiamua kuhamia kwingineko.

Akiongea na wanahabari baada ya mkutano wa faragha na wanachama wa kamati ya usalama na wale wa kitengo cha ujasusi, Bw Mohamed alisema maafisa hao tayari wamewatambua wakuu wa genge hilo.

Wakati wa operesheni iliyoendeshwa na maafisa wa usalama katika maficho yao, jumla ya simu 436 za mkono zilipatikana. Aidha, maafisa hao walipata tarakilishi 40, visu 67, mapanga 15, misokoto 3, 367 ya bangi na sachet kadha za dawa ya kulevya aina ya heroin.

Vile vile, walipata magwanda ya kijeshi, sare za maafisa wa shirika la vijana kwa huduma ya taifa (NYS), bunduki kadha bandia na pikipiki 10 zinazoshukiwa kutumiwa na wanachama wa genge hilo kuendeshea uhalifu.

“Tunaendesha uchunguzi ili kubaini iwapo wanachama wa genge la ‘confirm’ ndio walihusika katika mauaji ya wanawake eneo la Mawanga. Pia tunachunguza malengo yao au iwapo ni kundi lenye itikadi kali,” Bw Maalim akasema.

Tafsiri: CHARLES WASONGA

  • Tags

You can share this post!

Moraa na Korir mawindoni Stockholm Diamond League kinyume...

Ruto akubaliana na IEBC, Raila apinga

T L