Habari Mseto

GIKOMBA: Soko lenye historia ya mikasa ya moto

June 28th, 2018 1 min read

Na LUCY KILALO

SOKO la Gikomba Alhamisi lilishuhudia tukio baya zaidi katika miaka ya hivi karibuni ambapo moto uliangamiza maisha ya watu 15.

Katika miaka ya hivi punde, wafanyabiashara katika soko la Gikomba wamekuwa wakishuhudia hasara kubwa kufuatia matukio ya moto yanayoangamiza biashara zao.

Hali hiyo ilimchochea Rais Uhuru Kenyatta mnamo Oktoba 6 mwaka jana, kuagiza polisi kuchunguza kiini cha moto ulioharibu mali yenye thamani ya mamilioni katika soko hilo, tukio lingine lilipotokea.

“Tukio hili limewaathiri wafanyabiashara wengi kutoka kote nchini na uchunguzi unastahili kuzinduliwa kutafuta washukiwa na hatua kuchukuliwa dhidi yao,” rais alisema wakati huo akiwa anasaka kura katika Kaunti ya Meru katika uwanja wa Maua, Meru. Soko hilo lilichomeka moto ulipoanza saa tisa usiku.

Ingawaje kuna baadhi ya matukio ya awali ambayo yamehusishwa na nia ya kuzima biashara ya mitumba, katika miaka ya hivi punde mioto hiyo imeibua hisia tofauti kuhusiana na nia yake.

Mnamo Januari 15, 2009 mali yenye thamani ya mamilioni ilichomeka bila chanzo kamili kubainishwa.

Soko hilo ambalo ni kitovu cha biashara za kila aina na huvutia wafanyabiashara na wateja kutoka pembe zote nchini, pia liliathiriwa na moto mnamo Machi 2012, na baadaye Mei na Oktoba 2014, wafanyabiashara bado walikuwa wakikadiria hasara.

Mwaka uliofuata, Mei 2015 na pia Juni 2015, kulikuwa na matukio mengine ya moto ambayo yaliwasababishia hasara kubwa.

Mnamo Septemba na Oktoba 2017 pia mioto mingine ilishuhudiwa na kuibua maswali mengi kuhusiana na chanzo cha moto katika soko hilo.

Wafanyabiashara wamekuwa wakikumbwa na hasara kubwa, hali ambayo huwarudisha nyuma kimaisha.

Moto huo wa jana ulianzia sehemu inayotambulika kama Kwa Mbao panakaribiana na makazi, nyumba nyingi zikiwa zinamilikiwa na za Kaunti ya Nairobi.