Makala

GILBERT AWINO: Magereza yadhihirisha kilimo ni ngao dhidi ya ukosefu wa ajira

December 24th, 2020 2 min read

Na GILBERT AWINO

IJUMAA wiki ijayo tutakuwa tumeingia mwaka mpya wa 2021. Mwaka huu wa 2020 umeibuka kuwa mgumu sana kiasi kwamba haujawahi kuonekana mwingine kama huu katika kipindi cha karne moja iliyopita.

Unalinganishwa na mwaka wa 1918 ambapo janga la ugonjwa wa pumu lilikumba ulimwengu na kuangamiza hasa wanajeshi katika Vita Vya Pili Vya Dunia.

Tofauti ni kwamba wakati huo usafiri haukuwa wa kasi kama leo. Idadi ya watu ilikuwa ndogo na waliokuwa wakisafiri pia walikuwa wachache mno.

Utandawazi na maendeleo ya kiteknolojia tunayojivunia hii leo yameleta hatari zaidi, kwani janga likitokea linasambaa ulimwenguni haraka upesi.

Ni hali hiyo iliyochangia janga la virusi vya corona kuteka ulimwengu mzima katika miezi michache tu.Makali yake yanazidi kushuhudiwa siku baada ya nyingine.

Mamia ya maelfu wameaga dunia na mamilioni kuugua.Isitoshe, taarifa za serikali zaonyesha takribani watu milioni mbili wamepoteza kazi kutokana na janga hili.

Kampuni nyingi zilifunga, ikiwemo hoteli kubwa nchini kama Intercontinental na Radisson Blu. Faida za mabilioni ambazo benki zilikuwa zikijivunia kila mwaka ziliyeyuka.Hali imedhihirisha namna ambavyo mashirika makubwa hayakuwa yamejiandaa kukabiliana na majanga makubwa.

Hata hivyo, kuna taasisi moja ambayo imejizatiti kujikimu – magereza.Licha ya idadi kubwa ya wafungwa na mahabusu, magereza hayajapunguza idadi yao kwa sababu ya janga ama ukosefu wa chakula wala fedha.

Kila mwaka mfungwa mmoja hula karibu kilo 18 za nyama licha ya kwamba wafungwa hawazalishi wala kununua vyakula sokoni.Aidha wanakula takriban tani elfu moja ya chakula kila mwaka.

Kiini cha wao kuwa na lishe ya kutosha ni kwamba magereza yamebuni njia mbadala za kuhakikisha wanazalisha chakula na kujipatia mamilioni ya pesa kutokana na miradi yao mbalimbali ya kilimo, kama njia mojawapo ya kujikinga dhidi ya misukosuko ya kiuchumi jinsi inavyoshuhudiwa kwa sasa ulimwenguni.

Magereza yana miradi mikubwa kama vile ufugaji wa ng’ombe wa maziwa na nyama; na uzalishaji majani chai, mahindi na mazao mengine kwa lengo la kupata chakula na pia mazao ya kuuza ili kuokoa fedha kidogo wanzopewa na serikali.

Ripoti kutoka idara ya magereza nchini ilisema wanapanga kuokoa zaidi ya Sh 400 milioni kutokana na miradi hii ya kilimo. Pengine mashirika yatapuuza juhudi hizi za magereza kwa kisingizio kwamba nguvu kazi wanazotumia ni za bure.

Hata hivyo, maandalizi yao yanafaa kuigwa na mashirika makubwa; yangejiandaa vilivyo zaidi kwa majanga, kwa kuchangamkia kilimo, tungeokoa mamilioni ya ajira zilizotoweka.

Mashirika yaliyopata faida mwaka huu ni ya kilimo au yaliyoingilia biashara za kilimo. Kwa mfano, shirika la ndege la Kenya Airways lilizoa mapato yake kutokana na idadi kubwa ya bidhaa za kilimo, kama maparachizi, ambazo zilipata masoko mengi katika Milki za Kiarabu.

[email protected]