Michezo

Gini apata mtoto wa tatu

June 6th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

KIUNGO matata wa Liverpool na timu ya taifa ya Uholanzi, Georginio Wijnaldum, 29, sasa amekuwa dume kamili baada ya mkewe Virginia Braaf kujifungua mtoto wa kiume kwa jina Julian Emilio.

Wazazi wa Julian walimtambulisha rasmi kwa umma mnamo Juni 3, 2020 kupitia mtandao wa Instagram. Ujio wake unamfanya Wijnaldum ambaye tayari alikuwa akijivunia msichana Ki-Yean na mvulana Jacian, kuwa baba wa watoto watatu.

Wijnaldum anayehusishwa na uwezekano mkubwa wa kuhamia Bayern Munich ya Ujerumani mwishoni mwa msimu huu, alimvisha Virginia pete ya uchumba mnamo Februari 17, 2018 baada ya kutoka naye kimapenzi kwa zaidi ya miaka saba.

Akionekana kushindwa kabisa kudhibti furaha yake, Wijnaldum alipakia picha za kitoto chao mtandaoni na kuandika: “Ni fahari yangu kuwatangazia kuhusu kuzaliwa kwa kidume hiki, Julian Emilio mnamo Aprili 28, 2020!”

Wanasoka wengi walimtumia Wijnaldum na mkewe jumbe za heri na pongezi kwa kujaliwa mtoto. Baadhi yao ni chipukizi wa Liverpool, Rhian Brewster aliyesema: “Hongera sana kakangu kwa makombora mazito uliyofyatua. Siku zote nikidhani wewe ni bingwa tu uwanjani. Sasa nimetambua kwamba wewe ni jogoo chumbani vilevile.”

Patrick van Aanholt wa Crystal Palace na timu ya taifa ya Uholanzi alisema, “Kongole sana ndugu yangu kwa baraka nyingine.” Ujumbe wake ulishadidiwa na beki Nathaniel Edwin Clyne wa Liverpool na timu ya taifa ya Uingereza.

Wijnaldum ambaye amekuwa mhimili mkubwa katika mafanikio ya Liverpool katika kipindi cha misimu miwili iliyopita kwenye soka ya Uingereza na bara Ulaya (UEFA), angali na mkataba wa mwaka mmoja pekee uwanjani Anfield. Kandarasi hiyo itatamatika rasmi mnamo Juni 2021.