KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Giroud afikia rekodi ya Thierry Henry ya mfungaji bora wa muda wote kambini mwa Ufaransa

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Giroud afikia rekodi ya Thierry Henry ya mfungaji bora wa muda wote kambini mwa Ufaransa

Na MASHIRIKA

MABAO mawili yaliyofungwa na Olivier Giroud katika ushindi wa 4-1 uliosajiliwa na Ufaransa dhidi ya Australia mnamo Jumanne usiku ugani Al Janoub yalimweka katika mabuku ya historia.

Mvamizi huyo wa AC Milan aliifikia rekodi ya kigogo Thierry Henry aliyewahi kufungia Ufaransa mabao 51 kutokana na mechi 123 na kuwa mfungaji bora wa muda wote wa kikosi hicho.

Giroud, 36, alitumia jumla ya michuano 115 kufikia rekodi hiyo ya Henry. Mvamizi huyo wa zamani wa Chelsea na Arsenal, sasa ana fursa nzuri ya kutumia makala ya 22 ya fainali za Kombe la Dunia nchini Qatar kuweka rekodi mpya ya ufungaji mabao kambini mwa Ufaransa.

Jeraha la paja lililomnyima nyota Karim Benzema uhondo wa kipute cha mwaka huu nchini Qatar linamfanya Giroud kuwa tegemeo kubwa la kocha Didier Deschamps katika safu ya mbele ya Ufaransa wanaojivunia pia maarifa ya Ousmane Dembele, Antoine Griezmann na Kylian Mbappe.

Benzema, 34, amekuwa na tatizo la paja la kushoto tangu Oktoba na atasalia mkekani pamoja na Lucas Hernandez, N’Golo Kante, Paul Pogba, Christopher Nkunku na Presnel Kimpembe kwa kipindi kizima cha Kombe la Dunia.

Giroud alinyanyua Kombe la FA mara tatu akivalia jezi za Arsenal kabla ya kuongoza Chelsea kutwaa ubingwa wa kipute hicho mnamo 2018. Alifunga bao lililosaidia Chelsea kupepeta Arsenal katika fainali ya Europa League mnamo 2019 na akawa sehemu ya kikosi kilichonyakulia Chelsea ufalme wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo 2021.

Aliingia katika sajili rasmi ya Milan mnamo Julai 2021 na kuzolea miamba hao ubingwa wa Ligi Kuu ya Italia (Serie A) katika msimu wake wa kwanza. Analenga sasa kufanya Ufaransa kuwa kikosi cha tatu baada ya Brazil na Italia kuwahi kunyanyua Kombe la Dunia mara mbili mfululizo.

Ufaransa waliopepeta Croatia 4-2 kwenye fainali za 2018 nchini Urusi, sasa wanajiandaa kuonana na Denmark mnamo Novemba 26 kabla ya kufunga kampeni za Kundi D dhidi ya Tunisia mnamo Novemba 30.

Kwa kukomoa Australia, Ufaransa walijiweka pazuri kuepuka nuksi ya 2002 ambapo waliweka rekodi duni ya kuwa mabingwa watetezi wa Kombe la Dunia walioaga kivumbi hicho katika hatua ya makundi bila kusajili ushindi wowote.

Aidha, walikiuka mkondo ulioandamwa na mabingwa watetezi wa awali wa Kombe la Dunia – Ujerumani (2014), Uhispania (2010) na Italia (2006) – waliodenguliwa kwenye makala yaliyofuata ya fainali hizo kwenye hatua ya makundi.

Hadi Ufaransa walipoteremkia Australia mnamo Jumanne, ni Brazil pekee, mnamo 2006, waliowahi kushinda mchuano wa kwanza wa Kombe la Dunia wakiwa mabingwa watetezi.

Huku Giroud akitamba, mkosi ulizidi kumwandama mvamizi mzoefu wa Poland, Robert Lewandowski, aliyepoteza fursa ya kufunga bao lake la kwanza katika historia ya Kombe la Dunia.

Penalti iliyochanjwa na nyota huyo ambaye amefungia Barcelona mabao 18 kutokana na michuano 19 ya msimu huu, ilipanguliwa na kipa Guillermo Ochoa, 37, katika mchuano wa Kundi C ulioshuhudia Poland ikiambulia sare tasa dhidi ya Mexico ugani 974.

Lewandowski aliyeagana na Bayern Munich mwishoni mwa msimu wa 2021-22, hakubahatika kufunga bao dhidi ya Senegal, Colombia na Japan katika Kundi H kwenye fainali za 2018 nchini Urusi.

Matokeo ya Poland dhidi ya Mexico yalisaza Saudi Arabia kileleni mwa Kundi C kwa alama tatu baada ya kutoka nyuma na kuduwaza Argentina kwa ushindi wa 2-1.

Saudi Arabia ndicho kikosi cha kwanza kisichotokea bara Ulaya kuwahi kupepeta Argentina katika mechi ya Kombe la Dunia baada ya Cameroon mnamo 1990. Hadi walipozamishwa na Saudi Arabia, vikosi vitatu vya mwisho kuwahi kuangusha Argentina katika Kombe la Dunia viliishia kunyanyua taji la kipute hicho au kutinga fainali – Ujerumani na Ufaransa walitawazwa wafalme mnamo 2014 na 2018 mtawalia huku Croatia wakiingia fainali.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Bidhaa zilizoundwa kwa maganda ya miwa, magazeti na vitabu...

Matibabu: Minet yaagizwa isuluhishe mzozo wake na walimu

T L