Michezo

Giroud akaribia rekodi ya ufungaji ya Thierry Henry kambini mwa Ufaransa

November 18th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

FOWADI Olivier Giroud aliikaribia rekodi ya ufungaji ya nguli Thierry Henry baada ya kupachika wavuni mabao mawili katika ushindi wa 4-2 uliosajiliwa na Ufaransa dhidi ya Uswidi katika UEFA Nations League mnamo Novemba 17, 2020.

Giroud alifunga katika kila kipindi na kufikia mabao yake hadi 44. Sasa anasalia na magoli saba pekee kufikia rekodi ya mwanasoka wa zamani wa Arsenal, Henry, katika enzi yake ya usogora.

Uswidi walichukua uongozi wa mapema katika mechi hiyo kupitia kwa Viktor Claesson aliyechuma nafuu kutokana na masihara ya beki Benjamin Pavard.

Ingawa bao la Robin Quaison katika dakika ya 88 lilipania kurejesha Uswidi mchezoni, chombo cha kikosi hicho ambacho kwa sasa kimeshuka hadi League B kwenye gozi la Nations League, kilizamishwa na fowadi chipukizi Kingsley Coman mwishoni mwa kipindi cha pili.

Ufaransa waliotawazwa mabingwa wa dunia mnamo 2014 nchini Urusi, sasa wamejikatia mojawapo ya tiketi nne za kufuzu kwa fainali za Nations League kwa pamoja na Uhispania. Ubelgiji wa Denmark kutoka Kundi A2 na Uholanzi au Poland kutoka Kundi A1 ndivyo vikosi vingine ambavyo huenda vikajiunga na Ufaransa na Uhispania.

Bao la kwanza la Giroud lilikuwa zao la ushirikiano mkubwa kati yake na Marcus Thuram ambaye ni mwanawe shujaa wa Ufaransa kwenye fainali za Kombe la Dunia za 1998, Lilian Thuram.

Mchuano huo ulikuwa wa kwanza kwa Thuram katika jezi ya timu ya taifa ya Ufaransa na akashirikiana vilivyo na beki matata wa Bayern Munich, Pavard aliyefanya mambo kuwa 3-1 katika dakika ya 36.

Goli la pili lililofumwa wavuni na Giroud lilichangiwa na chipukizi mahiri wa Paris Saint-Germain (PSG), Kylian Mbappe katika dakika ya 59. Mbappe nusura afungie Ufaransa bao la tano mwishoni wa kipindi cha pili ila akanyimwa nafasi ya wazi na kipa chaguo la kwanza la Everton, Robin Olsen.