KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Giroud avunja rekodi ya Thierry Henry na kuwa mfungaji bora wa muda wote wa Ufaransa

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Giroud avunja rekodi ya Thierry Henry na kuwa mfungaji bora wa muda wote wa Ufaransa

Na MASHIRIKA

OLIVIER Giroud aliweka rekodi ya kuwa mfungaji bora wa muda wote katika kikosi cha Ufaransa baada ya kufunga bao katika ushindi wa 3-1 dhidi ya Poland na kufuzu kwa robo-fainali za Kombe la Dunia mwaka huu nchini Qatar.

Fowadi huyo wa AC Milan ya Italia alipachika wavuni goli lake la 52 akivalia jezi ya Ufaransa na kuvunja rekodi ya kigogo Thierry Henry.

Bao hilo la Giroud aliyekuwa akichezea Ufaransa kwa mara ya 117, lilifungwa mwishoni mwa kipindi cha kwanza kutokana na krosi ya Kylian Mbappe aliyemtatiza pakubwa kipa wa Poland, Wojciech Szczesny.

Mabao mengine mawili ya Ufaransa ambao ni mabingwa watetezi wa Kombe la Dunia yalijazwa kimiani na Mbappe katika kipindi cha pili. Mbappe sasa anaongoza orodha ya wafungaji bora kwenye Kombe la Dunia mwaka huu kwa mabao matano.

Poland walipoteza nafasi nyingi za wazi kupitia kwa Piotr Zielinski aliyeshindwa kumzidi maarifa kipa Hugo Lloris wa Ufaransa. Robert Lewandowski alifuta machozi ya Poland kupitia mkwaju wa penalti mwishoni mwa kipindi cha pili.

Ufaransa sasa watavaana na Uingereza kwenye robo-fainali mnamo Disemba 10,2022 ugani Al Bayt. Uingereza walitinga hatua hiyo ya nane-bora baada ya kuzamisha chombo cha Senegal kwa mabao 3-0 uwanjani Al Bayt.

Giroud, 36, aliondoka Uingereza na kuyoyomea Italia kuvalia jezi za AC Milan baada ya kuchezea Arsenal na Chelsea kwa kipindi cha misimu 10. Alipachika wavuni mabao 14 katika mashindano yote ya msimu jana na kuongoza waajiri wake kunyanyua taji la Serie A kwa mara ya kwanza baada ya miaka 11.

Ufaransa watashuhudia rekodi yao nyingine ikivunjwa iwapo kipa Lloris atawajibishwa dhidi ya Uingereza kwenye robo-fainali. Kipa huyo tayari amewajibikia Ufaransa mara 142 na mechi ijayo ya robo-fainali itamshuhudia akivunja rekodi ya kigogo Lilian Thuram.

Kwa kufunga mabao mawili, Mbappe alivunja rekodi ya Pele aliyefunga mabao saba kwenye Kombe la Dunia kabla ya kufikia umri wa miaka 24. Mbappe ambaye atafikisha umri wa miaka 24 siku mbili kabla ya fainali ya Kombe la Dunia mwaka huu, sasa ana mabao tisa kutokana na michuano 11.

Nyota huyo wa zamani wa AS Monaco sasa amepachika wavuni magoli 16 kutokana na mechi 14 zilizopita akiwajibikia Ufaransa na anajivunia jumla ya mabao 33 kutokana na michuano 63.

Poland sasa hawajashinda mechi yoyote kati ya nane zilizopita dhidi ya Ufaransa waliokung’uta Croatia 4-2 miaka minne iliyopita nchini Urusi na kujizolea ubingwa wa dunia kwa mara pili katika historia.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO 

You can share this post!

WANDERI KAMAU: Lilikuwa kosa kuwaogofya wanafunzi wa Gredi...

Makanisa yamtaka Raila azime maandamano aliyotangaza...

T L