Makala

'Githeri Man' hufuga kuku wa kienyeji, japo si wa biashara

March 8th, 2019 2 min read

Na SAMMY WAWERU

MARTIN Kamotho Njenga alipata umaarufu wakati wa uchaguzi mkuu wa 2017 kwa kula pure ‘githeri’ kwenye foleni.

Picha zake zilienea mitandaoni, vyombo vya habari vikimuangazia kwa kile kilitajwa kama mmoja wa Wakenya walioonesha uzalendo kushiriki shughuli hiyo ya kidemokrasia bila kubabaishwa na miale kali ya jua lilikuwa limechomoza kisawasawa.

Bw Kamotho maarufu kama ‘Githeri Man’ pia alipata tuzo ya HSC, inayopewa Wakenya walioafikia makubwa katika jamii.

Licha ya kushikwa na minyororo ya unywaji wa pombe kupindukia kiasi cha kupelekwa katika kituo kimoja cha kubadilisha mienendo na tabia Kiambu, Kamotho ni mfugaji wa kuku wa kienyeji.

Martin Kamotho Njenga maarufu kama ‘Githeri Man’, pia ni mfugaji wa kuku wa kienyeji mtaa wa Kayole, Nairobi. Picha/ Sammy Waweru

Hata ingawa shughuli hii haifanyi kwa minajili ya biashara, anasema ana mapenzi ya dhati kwa ndege hawa kwa kuwa huchangamsha boma lake.

“Ninapenda kuku sana, fahari yangu ni kuwaona kila asubuhi niraukapo na jioni nikitoka kwa shughuli za kutwa nzima,” anadokeza.

Anafanya kazi katika kaunti ya Nairobi, chini ya halmashauri ya jiji.

“Wangu ninawafuga wakiwa wa kula pekee, ambapo msimu wa Krismasi huwapa majirani. Huwa siwauzi, Mungu amenijaalia hivyo basi hurudisha shukrani kwa kuwapa bila malipo,” afafanua.

Mtaji

‘Githeri Man’ ambaye ni mzawa wa Githunguri, Kiambu, alianza ufugaji mwaka 2005 kwa kuku wawili pekee, mmoja mtamba na wa pili jogoo.

Anafichua kwamba iligharimu Sh1,200 kufungua jamvi la shughuli hii.

“Kila mmoja niliuziwa Sh600. Kizimba nilijiundia,” asema.

Wakati wa mahojiano na katika makazi yake mtaa wa Kayole, Nairobi, tulimpata akiwa na zaidi ya kuku 25.

Alisema kuku wa kienyeji hasa wale asilia ni rahisi mno kuwaweka kwa sababu huweza kujitafutia lishe wanapofunguliwa kujivinjari.

Isitoshe, masalia ya chakula cha binadamu kama ukoko wa ushumbi wa ugali, mboga, na hata majani ya nyasi ni mlo wao. Wanachohitaji zaidi ni kutiliwa maji kwa wingi, na katika vifaa safi.

Uwekezaji

Kuna baadhi ya wafanyakazi walioajiriwa kazi za ofisi na wanatumia akiba yao kuwekeza katika miradi mbalimbali ya kilimo na ufugaji, ili kupata kipato cha ziada.

Kwa kuwa Bw Kamotho amejaaliwa ajira na kuonekana kuwa na mapenzi ya kuku, anashauriwa kutumia nafasi hiyo ya kipekee kujiimarisha kimapato.

“Ukulima na ufugaji ndio uti wa mgongo wa nchi hii, ikiwa una nafasi ya kuuendesha usisite kuufanya. Wengi wameacha gange za kuajiriwa ili kufanya kilimo kwa kuwa kina mapato, taifa linahitaji chakula cha kutosha,” ahimiza James Kimemia, mtaalamu wa kilimo na ufugaji.

Maisha ya uzeeni hutegemea yale ya ujana, ni busara kwa Kamotho kuacha unywaji wa pombe ili aimarishe ufugaji na huenda mapenzi yake kwa kuku yakanenepesha mradi huo uwe mojawapo ya kitega uchumi chake mbali na mshahara anaopokea.

Yai la kuku wa kienyeji Nairobi hugharimu Sh20, na hii ina maana akitilia maanani ari yake awe na zaidi ya kuku 30 wanaotaga kila siku hatakosa kuuza kreti moja kwa Sh600.

Pili, kuku wa kienyeji msimu wa Krismasi nchini hawanunuliki, bei ya koo haipungui Sh1,000. Aidha, jimbi huuzwa hata zaidi ya Sh1,500.

Veronica Kyalo, ni mfugaji wa kuku wa kienyeji wa kisasa almaarufu Kuroiler, Kajiado na Kiambu.

Mama huyu anayewafuga kwa minajili ya mayai na nyama, aliacha kazi katika shirika la takwimu za kitaifa, KNBS, ili kuvalia njuga ufugaji wa kuku.

“Bei ya mayai kwa sasa ni duni kwa sababu ya yanayotoka mataifa ya nje. Hata hivyo, sijutii kufanya kilimo cha kuku kwani faida ninayopata inapiku mshahara niliokuwa nikilipwa,” anaeleza Bi Kyalo.

Anahimiza wenye nafasi tosha mijini kuwekeza katika ufugaji wa kuku wa kienyeji.

Mjasirimali huyu pia huuza vifaranga.

Kamotho akiiga mfano huu, kupata soko la mazao haitakuwa kizungumkuti, ikizingatiwa kuwa ni raia maarufu nchini na mwenye uhusiano wa karibu na Rais.

Ni vyema kumkumbusha miaka inazidi kusonga, uzee ukibisha hodi hivyo basi apevuke na kustawisha mradi wake wa kuku kabla kustaafu.