Michezo

Githurai Allstars yawatandika Makadara Juniors

July 22nd, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

MELTAH Kabiria iliiponda Kawangware United kwa magoli 4-0 huku Githurai Allstars ikijiongezea matumaini la kubeba ubingwa wa taji la Super Eight Premier League (S8PL) ilipotandika Makadara Junior League SA kwa mabao 2-0 uwanjani Stima Club, Nairobi.

Githurai Allstars ya kocha Evans Odenyo inayoshiriki kipute hicho kwa mara ya kwanza ilionyesha mechi safi ikipania kuvuna alama zote na kufanya kweli kupitia Stanley Kisoe na Joe Abong’o waliotisa wavu mara moja kila mmoja.

”Bila shaka napongeza wachezaji wangu maana wanaendelea kuzingatia azma yetu kwenye kampeni za msimu huu.”

Kawangware United inayojivunia kutwaa taji hilo mara moja ilijikuta kwenye wakati mgumu baada ya Dalton Musa kupiga kombora mbili safi huku kipindi cha Collins Omondi akitokea benchi na kuitingia mabao mawili.

Matokeo hayo yalifanya Meltah Kabiria ambayo hutiwa makali na kocha, Paul Kamau kusalia katika nafasi ya tatu kwa kuzoa alama 29, sawa na Mathare Flames iliyokaushwa kwa mabao 2-0 na Dagoretti Former Players. Nayo Jericho Allstars iliachia alama mbili muhimu ilipoagana sare tasa na MASA.

Githurai Allstars ambayo imeibuka kati ya vikosi vinavyotisha washiriki wengine katika ngarambe hiyo imekamata mbili bora kwa kuzoa 31 huku Jericho Allstars ikiwa kifua mbele kwa alama 33.

Kwenye mfululizo wa matokeo hayo, NYSA iliibana Shauri Moyo Sportiff kwa goli 1-0, Metro Sports ililambishwa sakafu ilizabwa mabao 3-2 na Huruma Kona nao wasomi wa TUK walimaliza sare tasa na Team Umeme.