Habari Mseto

Giza latanda Thika Road saa kadhaa

February 19th, 2020 1 min read

Na SAMMY WAWERU

SHUGHULI za biashara Jumanne jioni mitaa iliyoko pembezoni mwa Thika Superhighway zilitatizika kwa muda wa saa kadhaa kufuatia kupotea kwa nguvu za umeme.

Hitilafu hiyo iliyotokea mwendo wa saa moja iliathiri maeneo ya Ruaraka, Zimmerman, Githurai 44 na 45 na vilevile Kahawa West.

Maeneo mengine kwa mujibu wa chapisho la kitengo cha huduma za wateja cha kampuni ya Kenya Power PLC kwenye mitandao yake, ni Kahawa Wendani, Kahawa Sukari, Chuo Kikuu cha Kenyatta ndicho KU, Kasarani, Ruiru, Two Rivers, Devki Ruiru, Bidco Ruiru na mazingira ya Thika Superhighway.

“Tuna hitilafu katika kituo cha kusambaza nguvu za umeme cha Ruaraka, tunaomba radhi. Hata hivyo, tunashughulika kurejesha huduma kawaida,” kampuni hiyo ikaeleza.

Wenye magari Thika Superhighway walilazimika kupunguza kasi, kwa kuwa mataa ya barabara pia yalikuwa yamezimika. Honi zilisikika kutoka kwa magari yaliskika yakipiga honi ili kutadharisha yaliyo nyuma au mbele.

Hali ya kawaida ilirejea dakika chache kabla ya saa tatu za usiku. Wafanyabiashara wengi hawakuwa na budi ila kufunga maduka yao. Nguvu za umeme zinapopotea, visa vingi vya uhalifu huripotiwa.