Siasa

Godoro la UDA laendelea kuumiza walaliaji

June 5th, 2024 3 min read

NA MWANGI MUIRURI

MBUNGE wa Embakasi Kaskazini Bw James Gakuya, ambaye ni mfuasi sugu wa Naibu Rais Rigathi Gachagua, amesema kwamba chama cha Rais William Ruto cha United Democratic Alliance (UDA) kiko katika kitanda chake cha mauti kikiwa hali mahututi na huenda hivi karibuni washirika wacho kutoka Mlima Kenya wakajiondoa.

Bw Gakuya alisema kwamba “sisi watu wa Gachagua hatujalalia masikio na kwanza tunavipa vita ambavyo viko ndani ya UDA macho tu kama kipaumbele tukilenga kujifahamisha na hali itakavyokuwa na hatimaye ndio ikibidi, tuwaonyeshe makali yetu ya kumenyana miereka hiyo”.

“Lakini mambo yakichacha, hata tunaweza tukatoka kabla ya 2027,” akasema Bw Gakuya.

Bw Gakuya alisema Rais Ruto baada ya kunusa hali ya hatari kutoka Mlima Kenya amesimamisha uchaguzi wa chama cha UDA katika Kaunti ya Nairobi ambapo kulikuwa kuchaguliwe mwenyekiti wa Kaunti hiyo mnamo Ijumaa ijayo ya Juni 7, 2024.

“Tuko na uhakika kwamba katika uchaguzi huo wa mashinani kambi ya Bw Gachagua ilipata wajumbe 248 kati ya wote 340. Ina maana kambi hiyo nyingine inayoongozwa na Gavana Johnson Sakaja iko na wajumbe 92. Rais Ruto amenusa hatari iliyoko kwamba tutamwangusha Bw Sakaja na ndipo ametwambia kwamba kwanza tuahirishe uchaguzi wa mwenyekiti akisema kwamba akirejea kutoka ziara yake ya Korea Kusini angetaka kuongea na wawaniaji,” akasema Bw Gakuya.

Bw Gakuya alisema kwamba anaona hiyo ikiwa ni njama inayosukwa ya kupanga namna ya kubatilisha matokeo ya uchaguzi huo wa UDA “na ninataka kutangaza kwamba ikiwa rais atajaribu hilo, basi atajua hata sisi sio wa kuhadaiwa”.

Alisema kwamba Mlima Kenya uliamua kimakusudi kuwania nyadhifa za UDA “ndio tujue heshima waliyo nayo nasi wenyeji wa Mlima Kenya inaangushia uzani katika ratili kwa kiwango kipi”.

Alisema ikiwa demokrasia haitapewa nafasi ya kujidhihirisha katika uchaguzi huo wa mashinani wa UDA, “basi tutajua hatuna chama, hakuna heshima, wamepata washirika wapya na wako huru kuendelea nao nasi sisi tukikanyaga kubwakubwa kuweka chama chetu kipya sokoni”.

Bw Sakaja naye amekuwa akisema kwamba alipata wajumbe 240 katika uchaguzi huo wa mashinani Nairobi na kumwachia Bw Gakuya na washirika wake–makombo ya wajumbe 100–ikiwa na maana kwamba yeye anatarajia kutawazwa mwenyekliti wa UDA Nairobi.

Aidha, amekuwa akisema kwamba hakupewa wadhifa wake na yeyote katika uchaguzi wa Agosti 9, 2022, kama ilivyogeuka mazoea ya siku za hivi majuzi ya wandani wa Bw Gachagua kudai, akisisitiza kwamba alichaguliwa katika debe na kura zikahesabiwa ambapo alitangazwa rasmi kuwa mshindi.

Alisema kwamba “kuna huyu Katibu Mkuu wa chama ambaye aliletwa kwa jina Cleophas Malala na ambaye hakuna hata jasho alimwaga kuunda chama hicho lakini akatolewa kutoka kile chao cha Amani National Congress (ANC) chake Mkuu wa Mawaziri na Waziri wa Masuala ya Kigeni Musalia Mudavadi na akatwikwa jukumu ndani ya chama chetu”.

Alisema kwamba kazi ya Bw Malala katika majukumu yake imekuwa tu ya kuzidisha uhasama na kudgarau wengine huku akijitwika mamlaka yasiyo yake kwa kuwa “hata hakuna mtu a,mbaye ameidhinisha kazi hiyo yake bali ni kushikilia anashikilia”.

Bw Gakuya akiwa katika mahojiano na kituo cha redio cha Kameme FM ambacho kinamilikiwa na Rais mstaafu Uhuru Kenyatta, alisema kwamba “kwa sasa hakuna kazi nyingine Malala anafanya isipokuwa ile ya kuwafuta kazi watu wa Mlima Kenya kutoka UDA na kuajiri wale wa kutoka kwao pia nayo serikali kuu ikiwatoa wetu wa Mlimani kutoka nyadhifa zilizo na upokezi wa rasilimali za wafadhili na kuwaweka wa kutoka kwao ili watumike katika wizi wa fedha hizo”.

Alisema ikiwa hujuma hizo zitaendelea, wandani wa Bw Gachagua watatafakari upya uhusiano wao na chama cha UDA na pia mikataba yoyote ya 2027.

“Ni lazima sisi watu wa Mlima Kenya tuanze kuongea kwa sauti moja tukijiandaa kufanya maamuzi magumu kuziba hali ya matanga ya siasa ambayo tunapangiwa,” akadai.

Alisema malumbano ndani ya UDA yako katika kiwango cha juu na wandani wa Bw Gachagua kwa sasa wanadai heshima yao ya asilimia 47 ya serikali kwa mujibu wa kura zao ambazo zilikuwa 87 kutoka Mlima Kenya.

“Kwa sasa vita viko na sisi tunalenga kutwaa jiji la Nairobi liwe liwalo kutoka kwa utawala wa Bw Sakaja ambao haujielewi. Hatimaye katika kura ya Mswada wa Fedha wa 2024, sisi wa Mlima tutaupinga kwa dhati iwapo vipengele tata vya kuzua ushuru kiholela havitafanyiwa marekebisho,” akasema.

Alionya wale wa kutoka Mlima Kenya ambao kazi yao ni kutumiwa kuhujumu umoja wa eneo hilo na uthabiti wa Bw Gachagua katika siasa za kitaifa na eneo, wajiandae kwa vita kamili nyanjani.

Bw Gakuya alisema kwamba siasa hizo za kupigana na Bw Gachagua zimefathiliwa katika Kaunti za Kiambu, Kirinyaga na Laikipia “na wanaowapea mawe ya kupiga mwenzao sio wengine bali ni wale tuliowaamini na kura zetu”.

Alisema “sisi watu wa Mlima Kenya tuko katika mkondo wa kugundua kwamba wema wetu unatumiwa vibaya kwa kuwa tuko safari moja na washirika ambao ni kama wamebeba visu na tukifika kwa giza wanatumalizia mmoja mmoja”.

Bw Gakuya alisema kwamba kwa sasa wapigakura wa Mlima Kenya wanajuta kumpigia Bw Sakaja kura “na kwamba hata tungempigia yule wetu wa Azimio ambaye ni Polycarp Igathe kama vile wale wao walimnyima wetu kura na wakampea wao kwa usaidizi wetu”.