Michezo

Gogo Boys yapania kuwa na makali ya Gor

March 23rd, 2020 2 min read

Na JOHN KIMWERE

GOGO Boys inapania kujituma mithili ya mchwa kupigania tiketi ya kupandishwa ngazi kushiriki kipute cha Ligi ya Taifa Daraja la kwanza muhula ujao.

Gogo Boys ambayo hutiwa makali na kocha, Wilburforce Chisira ni kati ya vikosi vinavyotikisa kwenye kampeni za kipute hicho msimu huu.

Gogo Boys inayoshiriki mechi za Kundi A Ligi ya Taifa Daraja la Pili kwa mara ya kwanza bila kusahau Kibera United na Ruiru Hotstars zote zimeonyesha wazi kuwa zinakuja kwa kasi kwenye kampeni za kipute cha msimu huu.

Mlenzi wake, Dkt Ahmed Kalebi anasema ana furaha tele kwa jinsi vijana wake wanavyojitahidi kiume kufukuzia tiketi ya kushiriki soka la hadhi ya juu muhula ujao.

”Kusema kweli tunalenga kutifua vumbi la kufa mtu kwenye jitihada za kusaka nafasi ya kusonga mbele,” anasema na kuongeza kuwa kampeni hizo sio mteremko.

Wafuasi wa Gogo Boys wakishabikia timu yao. Picha/ John Kimwere

Anadokeza kuwa kikosi chake kimekaa vizuri kuvuruga wapinzani wao na kufanya kweli. Anatoa mwito kwa wachana nyavu wake kutolaza damu dimbani pia wamakanike vilivyo ili kutimiza azma yao.

Kadhalika anasema atakuwa mwenye furaha zaidi endapo Gogo Boys itafanikiwa kuibuka bingwa wa kipute hicho na kutia kapuni tiketi ya kupanda ngazi.

GOR MAHIA NA AFC LEOPARDS

Mwenyekiti wake, Abdul Suleiman anashukuru wafuasi wa kikosi hicho kwa kujitolea mhanga kukipigia debe kwenye juhudi za kutafuta ubingwa huo.

”Ingawa Gogo Boys inashiriki mechi za kiwango cha chini tayari imevutia mashabiki wengi kama ilivyo kwa klabu za Ligi Kuu ya KPL zilizokongwe hapa nchini Gor Mahia na AFC Leopards,” alisema. Aliongeza kuwa idadi kubwa ya wafuasi wao imewatia motisha zaidi wachezaji wa kikosi hicho michezoni.

Baadhi ya wachezaji wa Utafiti FC inayoshiriki kipute hicho. Picha/ John Kimwere

LIGI KUU YA KPL

Mwenyekiti huyo anasema Gogo Boys ya mtaani Kibera, Kaunti ya Nairobi pia inataka kupambana mwanzo mwisho ikilenga kufuzu kushiriki Ligi Kuu miaka ijayo.

Aidha inakusudia kukuza talanta za wachezaji wengi tu wafuzu kuteuliwa kupigia timu ya taifa ya Harambee Stars siku sijazo.

Katika mpango mzima inajivunia kunoa makucha ya wanasoka kadhaa ambao wamebahatika kusajiliwa kuzipigia timu tofauti zinazoshiriki ligi mbali mbali nchini.

Dkt Ahmed Kalebi, mlezi wa Gogo Boys. Photo/ John Kimwere

Gogo Boys inategemea wachana nyavu ambao wameibuka kaa la moto wakishuka dimbani wakiongozwa na nahodha huyo, Yusuf Ali, Khubeib Ali, Hillary Shirao kati ya mafundi wa kutupia kambani mabao sio haba, Kelvin Senya, Gilbert Omondi na Collins Idapa.

Klabu hii ilibuniwa mwaka 2010 azma kuu ikiwa kuzima na kubadilisha mienendo ya vijana wengi mtaani. Hata hivyo ukosefu wa udhamini umechangia mtaa wa kibera kupoteza vijana wengi wenye utajiri kubwa katika mchezo wa soka na michezo mingineyo.