Michezo

GOLD COAST AUSTRALIA: Kenya kuzidi kusaka dhahabu

April 12th, 2018 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

NISHANI ya dhahabu ilizidi kuwa telezi hapo Jumatano kwa kikosi cha riadha kinachopeperusha bendera ya Kenya katika makala ya 21 ya Michezo ya Jumuiya ya Madola inayoendelea jijini Gold Coast, Australia.

Hii ni baada ya Wakenya Fancy Cherono, Purity Cherotich Kirui na Celliphine Chepteek Chespol kuzidiwa maarifa na mtimkaji mzawa wa Jamaica, Aisha Praught, aliyetawala fainali ya mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji.

Chespol aliridhika na nishani ya fedha baada ya kukamilisha mbio hizo kwa muda wa dakika 9:22.61 nyuma ya Praught aliyejizolea dhahabu kwa kukata utepe mwishoni mwa dakika 9:21.00.

Kirui aliambulia medali ya shaba baada ya kusajili muda wa dakika 9:25.74 na kumpiku mwanariadha mzawa wa Uingereza, Rosie Clarke aliyemaliza katika nafasi ya nne kwa muda wa dakika 9:36.29.

Licha ya kusajili muda bora na wa kasi zaidi katika kampeni za msimu huu (9:46.27), Cherono aliambulia nafasi ya sita nyuma ya mwanaridha mzawa wa Australia, Genevieve Lacaze aliyefunga orodha ya tano-bora wa muda wa dakika 9:42.69.

Lennie Waite wa Scotland alivuta mkia wa fainali hiyo kwa muda wa dakika 10:21.72, nyuma ya Genevieve Lalonde (dakika 9:46.68, Canada), Iona Lake (dakika 9:58.92, Uingereza) na Victoria Mitchell (dakika 10:12.59, Australia).

Hadi kufikia sasa, Kenya imejizolea jumla ya medali sita baada ya kujitwalia nishani za shaba mnamo Jumapili iliyopita kupitia kwa mwanafunzi wa Kidato cha Nne, Edward Zakayo (mita 5,000) na Samuel Gathimba aliyetia fora katika matembezi ya kilomita 20.

Kipusa Stacy Ndiwa aliishindia Kenya nishani ya fedha mnamo Jumatatu katika mbio za mita 10,000 kwa upande wa wanawake zilizotawaliwa na mwanariadha wa Uganda, Stella Chesang’ aliyeandikisha muda wa dakika 31:45.30.

Watimkaji Sandrafelis Chebet na Beatrice Mutai waliotumainiwa kuzolea Kenya nishani nyinginezo katika mbio hizo za mita 10,000 waliambulia nafasi za nne na 10 kwa muda wa dakika 31:49.81 na 32:11.92 mtawalia.

Beatrice Chepkoech aliivunia Kenya medali ya pili ya fedha mnamo Jumanne baada ya  kumtoa kijasho bingwa wa Afrika Kusini, Caster Semenya aliyejizolea dhahabu katika mbio za mita 1,500 kwa upande wa wanawake.

Kenya ina fursa ya kujiongezea medali zaidi hii leo wakati Aron Kipchumba Koech na bingwa wa dunia Nicholas Kiplagat Bett watakaponogesha fainali ya mbio za mita 400 kuruka viunzi.

Isitoshe, Wakenya Jonathan Kitilit na Wycliffe Kinyamal watategemewa sana kunyakulia Kenya nishani muhimu katika fainali ya mbio za mita 800 kwa upande wa wanaume.