Michezo

GOLD COAST AUSTRALIA: Lionesses wamumunywa kama pipi na New Zealand

April 14th, 2018 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

LIONESSES ya Kenya imeanza kampeni yake ya raga ya wachezaji saba kila upande ya Michezo ya Jumuiya ya Madola kwa kunyolewa bila maji 45-0 dhidi ya New Zealand mjini Gold Coast, Ijumaa.

Warembo wa kocha Kevin Wambua walizidiwa nguvu, mbio na hata maarifa katika vipindi vyote viwili na kupoteza mchuano huo wa Kundi A kupitia miguso ya Portia Woodman (mitatu), Nial Williams (miwili), Gayle Broughton (moja) na Kelly Brazier (moja). Tyla Nathan-Wong alipachika mikwaju mitano kati ya sita aliyopiga.

Zilipokutana na kwa mara ya kwanza katika Michezo ya Olimpiki jijini Rio de Janeiro, Brazil, mwaka 2016, Kenya ilipapurwa 52-0 na New Zealand katika mechi za makundi. Inamaanisha kwamba Kenya bado haijapata kufunga alama yoyote dhidi ya mabingwa hawa mara nne wa Raga za Dunia.

Mechi ijayo ya Kenya itakuwa dhidi ya Canada saa sita na dakika 11 adhuhuri. Canada ilinyuka mabingwa wa Afrika, Afrika Kusini 29-0 katika mechi yake ya ufunguzi. Ilifunga miguso yake mitano kupitia Brittany Benn, Caroline Crossley, Hannah Darling, Sara Kaljuvee na Charity Williams. Nahodha Ghislaine Landry aliongeza mikwaju miwili.

Kenya itakamilisha mechi zake za makundi dhidi ya Afrika Kusini mnamo Aprili 14.