Michezo

Golikipa na nahodha wa Bayern Munich atia saini mkataba mpya wa miaka mitatu

May 20th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

KIPA Manuel Neuer wa Bayern Munich amerefusha mkataba wake na kikosi hicho cha Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) kwa miaka mitatu zaidi hadi Juni 2023.

Kufikia sasa, Neuer, 34, anajivunia kunyanyulia Bayern mataji saba ya Bundesliga, matano ya German Cup na moja la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) tangu ajiunge na miamba hao wa soka ya Ujerumani kutoka Schalke mnamo 2011.

Kwa mujibu wa Neuer ambaye ni nahodha wa Bayern, yeye “anajihisi nyumbani zaidi” akivalia jezi za waajiri wake wa sasa na anatazamia mambo mazuri zaidi kumtokea akiwa ugani Allianz Arena.

“Katika kipindi ambapo shughuli zote za soka zilikuwa zimesitishwa nchini, nisingeweza kabisa kufanya maamuzi yoyote kuhusu mustakabali wangu kitaaluma,” akatanguliza.

“Kwa sababu sasa hali ya ukawaida inaendelea kurejelewa na kipute cha Bundesliga kuanza upya, natazamia siku za halafu ambazo zitaleta matumaini zaidi kwa sababu Bayern ni miongoni mwa vikosi bora zaidi katika soka ya bara Ulaya,” akasema Neuer.

Hadi kufikia sasa, Neuer anajivunia kuchezea timu ya taifa ya Ujerumani jumla ya mechi 92 na alikuwa tegemeo kubwa katika fainali kambini mwa kikosi hicho katika fainali za Kombe la Dunia zilizotawaliwa na Ujerumani mnamo 2014 nchini Brazil.

Japo amekuwa chaguo la kwanza la Bayern kwa kipindi kirefu, Neuer atalazimika kukabiliana na ushindani mkali wa kuhifadhi nafasi yake katika kikosi cha kwanza msimu ujao baada ya kusajiliwa kwa chipukizi Alexander Nubel, 23, kutoka Schalke.

Nubel ambaye ni mchezaji wa zamani wa kikosi cha U-21 katika kikosi cha Ujerumani, ametia saini mkataba wa miaka mitano na Bayern.