Google kufuta jumbe potovu kuhusu chanjo ya corona YouTube

Google kufuta jumbe potovu kuhusu chanjo ya corona YouTube

Na MARY WANGARI

KAMPUNI ya Google kupitia mtandao wake wa kijamii wa video wa YouTube, imezindua sera mpya inayopiga marufuku matini zote zinazoeneza uvumi kuhusu chanjo ikiwemo dozi za Covid-19.

Miongoni mwa matini zitakazoondolewa na mtandao huo unaomilikiwa na kampuni ya Google ni pamoja na video zinazodai kuwa chanjo zilizoidhinishwa na wizara ya afya ni hatari, hazifai, husababisha maradhi kama vile saratani na aina nyingine ya porojo.

Kando na chanjo dhidi ya virusi vya corona, sera hiyo mpya itahusisha chanzo zilizoidhinishwa na ambazo zimekuwa zikitumika kwa muda sasa dhidi ya maradhi kama vile ukambi na hepatitis B.

“Tunapanua sera zetu kuhusu uenezaji wa porojo kuhusu chanjo ambazo zimeidhinishwa na kuthibitishwa kuwa salama na wizara za afya na Shirika la Afya Duniani (WHO),” alisema Naibu Rais wa YouTube katika Idara ya Imani na Usalama wa Dunia, Matt Halprin Jumatano, Septemba 30.

Alifafanua kuwa sera hiyo mpya itaruhusu matini kuhusu majaribio mapya ya chanjo, sera za chanjo, simulizi za watu binafsi, video zinazosimulia matukio ya kihistoria kuhusu chanjo zilizofanikiwa na zile zilizofeli, kuendelea.

“Tutaondoa matini zinazoshenei madai kuwa chanjo ni hatari au zinasababisha madhara mengi ya kiafya, kwamba zinasababisha autism, saratani, ugumba au zinasheheni vifaa vya kielektroniki,”

“Mamia ya wataalam wa kudhibiti matini katika You Tube wanaangazia hasa uenezaji uvumi kuhusu masuala ya matibabu,” alisema.

Sera hizo mpya zitatekelezwa katika lugha zote zinazotumika kwenye mtandao huo wa YouTube.

Hatua hiyo imejiri miezi kadhaa baada ya marufuku sawia kutangazwa Februari na Facebook na nyingine iliyotangazwa na Twitter mnamo Machi, inayolenga uenezaji habari potofu kuhusu chanjo za maradhi mbalimbali.

Matukio haya ya hivi majuzi yameashiria mkondo mpya katika sera za utekelezaji ambazo zimeshikiliwa kwa muda na mitandao ya kijamii kuhusu sheria kali za kudhibiti matini.

Awali, YouTube ilikuwa imehoji kuwa mitandao wazi isiyodhibitiwa ni muhimu mno katika kuwezesha uhuru wa kuzungumza.

You can share this post!

Uhitaji wa jezi ya Ronaldo waongezeka kwa asilimia 3,000

Lewandowski afunga mabao mawili na kuongoza Bayern...